04. at-Twahaawiyyah anawaraddi wale Hanafiyyah waliokuja baadaye

Mwandishi ameandika kitabu hiki kwa mujibu wa madhehebu ya Ahl-us-Sunnah kwa ujumla. Miongoni mwao ni Imaam Abu Haniyfah an-Nu´maan bin Thaabit al-Kuufiy. Yeye ndiye alikuwa wa kwanza katika wale maimamu wane wanaotambulika, alikutana na Taabi´uun na akapokea kutoka kwao. Kadhalika wanafunzi wake wawili Abu Yuusuf na Muhammad ash-Shaybaaniy na maimamu wa madhehebu ya Hanafiyyah. Ametaja ´Aqiydah yao na kwamba ni yenye kuafikiana na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Hapa kuna Radd kwa wale Hanafiyyah wa leo na wa kale ambao wanajinasibisha kwa Abu Haniyfah lakini hata hivyo wanamkhalifu katika ´Aqiydah yake. Wanakubaliana naye katika Fiqh peke yake na wana ushabiki kwake. Wakati huohuo wanamkhalifu katika ´Aqiydah. Wanachukua ´Aqiydah ya wanafalsafa na watu wa mantiki. Kadhalika haya yametokea kwa Shaafi´iyyah; wanakwenda kinyume na Imaam ash-Shaafi´iy katika ´Aqiydah yake. Wanajinasibisha naye katika Fiqh pekee. Kadhalika wengi katika Maalikiyyah wametumbukia katika mtihani huu. Hawana ´Aqiydah ya Imaam Maalik, wanamfuata tu katika Fiqh. Ama inapokuja katika ´Aqiydah, ni wenye njia mbalimbali na mielekeo ya waliokuja nyuma.

Kwa hivyo kitabu hiki ni Radd kwa watu hawa na mfano wao katika wale ambao wanajinasibisha na maimamu wanne na wanafuata madhehebu yao licha ya kuwa ni wenye kwenda kinyume nao katika ´Aqiydah.

Kitu kama hicho kinaweza kuonekana pia kwa Ashaa´irah; wanajinasibisha kwa Imaam Abul-Hasan al-Ash´ariy katika ´Aqiydah yake ya kwanza na wanayaacha yale aliyothibitisha na akayafuata mwishoni katika ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ujinasibishaji kama huu si sahihi. Kwa sababu lau kweli wangelikuwa wanafuata madhehebu ya maimamu basi wangelifuata pia ´Aqiydah zao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 04/06/2019