04. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya Vitabu na Mitume II

3- Nguzo ya tatu: Kuamini Vitabu ambavyo Allaah ameviteremsha kwa Mitume. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameteremsha Vitabu na akawatumiliza Mitume kutoka kwake Yeye (Subhaanah) vikiwa vimebeba Wahy Wake, Shari´ah Zake, maamrisho na makatazo Yake. Miongoni mwavyo ni Tawraat, Injiyl, az-Zabuur, Qur-aan na vipo vitabu vyengine ambavyo Allaah hakututajia sisi. Lakini hata hivyo tunaviamini kwa njia ya ujumla na tunaamini vile ambavyo Allaah ametutajia kwa majina kwa njia ya upambanuzi. Cha mwisho na kitukufu zaidi ni Qur-aan tukufu ambayo imewashinda majini na watu kuleta Suurah moja peke yake mfano wake.

4- Nguzo ya nne: Kuwaamini Mitume waliotumilizwa na Allaah kwa Shari´ah Yake na dini Yake kwa ajili ya kuwaongoza viumbe Wake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amewatuma Mitume ili kuwabainishia watu yale yenye kuwadhuru na yale yenye kuwanufaisha na wawabainishie dini yao. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesimamisha hoja kupitia wao:

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

“Mitume ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kuletwa Mitume hao.”[1]

Kuhusu idadi yao hakuna aijuaye isipokuwa Allaah. Ni wengi. Miongoni mwao wako ambao Allaah ametutajia pale aliposema (Ta´ala):

وَتِلْكَ حُجَّتُنَا آتَيْنَاهَا إِبْرَاهِيمَ عَلَىٰ قَوْمِهِ ۚ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَّن نَّشَاءُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ كُلًّا هَدَيْنَا ۚ وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلْيَاسَ ۖ كُلٌّ مِّنَ الصَّالِحِينَ وَإِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطًا ۚ وَكُلًّا فَضَّلْنَا عَلَى الْعَالَمِينَ

“Na hiyo ndio hoja Yetu tuliyompa Ibraahiym juu ya watu wake.  Tunampandisha cheo tumtakaye. Hakika Mola wako ni Mwenye hekima, Mjuzi wa kila kiut. Na Tukamtunukia Ishaaq na Ya’quub – wote tuliwaongoza – na Nuuh tulimwongoza kabla na katika kizazi chake Daawuud na Sulaymaan na Ayyuub na Yuusuf na Musaa na Haaruun; na hivyo ndivyo tunavowalipa wenye kufanya ihsaan, na Zakariyyaa na Yahyaa na ‘Iysaa na Ilyaas – wote ni miongoni mwa waja wema, na Ismaa’iyl na al-Yasaa´ na Yuunus na Luutw – na wote tuliwafadhilisha juu ya walimwengu.”[2]

Hawa wametajwa na Allaah. Kwa hivyo tunatakiwa kuwaamini mmojammoja. Kuhusu wale ambao Allaah hakututajia tunapaswa kuwaamini kwa jumla. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ

“Hakika Tumewapeleka Mitume kabla yako; miongoni mwao wako Tuliokusimulia na miongoni mwao wako ambao hatukukusimulia.”[3]

Kwa hivyo tunawaamini wote kwa jumla ambao Allaah ametutajia na wale ambao Allaah hakututajia miongoni mwao. Yule mwenye kumkana Mtume mmoja basi amewakana wote. Kwa hivyo ni lazima kuwaamini wote:

إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا

“Hakika wale waliomkufuru Allaah na Mitume Wake na wanataka kufarikisha kati ya Allaah na Mitume Wake na wanasema: “Tunaamini baadhi [ya Mitume] na tunawakanusha wengine” na wanataka kuchukua njia iliyo baina ya hayo – hakika hao ndio makafiri wa kweli.”[4]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ametwambia:

قُولُوا آمَنَّا بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ

“Semeni: “Tumemuamini Allaah na yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl na Ishaaq na Ya’quub na kizazi na aliyopewa Muusa na ‘Iysaa na waliyopewa Manabii kutoka kwa Mola wao – hatutofautishi kati ya mmoja yeyote miongoni mwao; nasi Kwake ni wenye kujisalimisha.[5]

[1] 04:165

[2] 06:83-86

[3] 40:78

[4] 04:150-151

[5] 02:136

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 01/03/2021