04. ´Aqiydah sahihi juu ya Malaika wa Allaah

Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, kufufuliwa baada ya kufa na kuamini Qadar.

Imani ya kumuamini Allaah kumejumuisha kuthibitisha Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat, jambo ambalo tumeshatangulia kulitaja.

Imani ya kuamini Malaika ni kuthibitisha na kuamini uwepo wao, majina yao yaliyotajwa na matendo yao yaliyotajwa. Amesema (Ta´ala):

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ

“Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake na waumini. Wote wamemwamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Mitume Yake.” (02:285)

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ

“Si wema pekee kwa nyinyi kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi, lakini wema khaswa ni yule mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii.” (02:177)

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amepokea katika Hadiyth yake ndefu kuhusu swali la Jibriyl alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya imani. Akajibu ifuatavyo:

“Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar; kheri na shari yake.”

Allaah (Ta´ala) amewasifu katika Kitabu Chake ifuatavyo:

وَلَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَنْ عِندَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ

“Na ni Vyake pekee vyote vilivyomo katika mbingu na ardhi na wale walio Kwake hawatakabari na ‘ibaadah Yake na wala hawachoki. Wanasabihi usiku na mchana wala hawazembei.” (21:19-20)

وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَـٰنُ وَلَدًا ۗ سُبْحَانَهُ ۚ بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ

“Na wakasema: “Mwingi wa rehema Amejifanyia mwana.” Utakasifu ni Wake! Bali [hao Malaika] ni waja waliokirimiwa. Hawamtangulii kwa kauli nao kwa amri Yake wanafanya.” (21:26-27)

إِنَّ الَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيُسَبِّحُونَهُ وَلَهُ يَسْجُدُونَ

“Hakika wale walioko kwa Mola wako hawatakabari kufanya ‘ibaadah Yake na wanamsabihi na Kwake pekee wanasujudu.” (07:206)

Wao ni waja na viumbe miongoni mwa viumbe vya Allaah (Ta´ala) wakubwa. Malaika hawastahiki chochote katika ´ibaadah. Amesema (Ta´ala):

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ

“Na siku Atakayowakusanya wote kisha atawaambia Malaika: “Je, hawa ndio waliokuwa wakikuabuduni?” Watasema: “Utakasifu ni Wako! Wewe ni Mlinzi wetu pasi nao. Bali walikuwa wakiabudu majini, wengi wao wakiwaamini.”” (34:40-41)

وَلَا يَأْمُرَكُمْ أَن تَتَّخِذُوا الْمَلَائِكَةَ وَالنَّبِيِّينَ أَرْبَابًا ۗ أَيَأْمُرُكُم بِالْكُفْرِ بَعْدَ إِذْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Na wala hakuamuruni kuwafanya Malaika na Manabii kuwa miungu. Je, anakuamrisheni ukafiri baada ya nyinyi kuwa waislamu?” (03:80)

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amepokea ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika wameumbwa kutokana na nuru, majini wameumbwa kutokana na mwako wa moto na Aadam ameumbwa kutokana na kile kilichosifiwa kwenu.”

Miongoni mwa sifa zao ni kwamba wana mbawa. Katika wao kuna ambao wana mbawa mbili, wengine wana mbawa tatu, wengine wana mbawa nne na kusonga mbele. Amesema (Ta´ala):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۚ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Himdi zote ni stahiki ya Allaah muanzilishi wa mbingu na ardhi, Mwenye kuwafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbilimbili, tatutatu na nnenne. Huzidisha katika uumbaji Atakavyo – Hakika Allaah juu ya kila jambo ni Muweza.” (35:01)

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy kumepokelewa kutoka kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Jibriyl akiwa na mbawa mia sita.”

Allaah (Ta´ala) amewapa uwezo wa kuweza kujigeuza katika maumbile mazuri. Kama ambavyo Jibriyl (´alayhis-Salaam) alivyojigeuza kwa Maryam katika umbile la mtu kamilifu. Vivyo hivyo kama walivyojidhihirisha kama wageni wawili watukufu pindi walipomtembelea Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) na hali kadhalika wakafanya pindi walipomjia Luutw (´alayhis-Salaam) walipokuja kuteremsha adhabu kwa watu wake na mfano wa hayo.

Allaah amewakemea washirikina ambao wamedai kuwa Malaika ni wasichana wa Allaah – Allaah ametakasika na yale ambayo madhalimu wanasema. Amesema (Ta´ala):

وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَـٰنُ وَلَدًا ۗ سُبْحَانَهُ ۚ بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ

“Na wakasema: “Mwingi wa rehema Amejifanyia mwana.” Utakasifu ni Wake! Bali [hao Malaika] ni waja waliokirimiwa. Hawamtangulii kwa kauli nao kwa amri Yake wanafanya. Anajua yale yaliyoko mbele yao, na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawamuombei uombezi yeyote yule isipokuwa kwa yule ambaye amemridhia. Nao kutokana na kumkhofu ni wenye kutahadhari.” (21:26-28)

Baada ya hapo amesema (Ta´ala) kuhusu Malaika:

فَاسْتَفْتِهِمْ أَلِرَبِّكَ الْبَنَاتُ وَلَهُمُ الْبَنُونَ أَمْ خَلَقْنَا الْمَلَائِكَةَ إِنَاثًا وَهُمْ شَاهِدُونَ أَلَا إِنَّهُم مِّنْ إِفْكِهِمْ لَيَقُولُونَ وَلَدَ اللَّـهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ أَصْطَفَى الْبَنَاتِ عَلَى الْبَنِينَ مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ أَمْ لَكُمْ سُلْطَانٌ مُّبِينٌ فَأْتُوا بِكِتَابِكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Waulize: “Je, Mola wako ndio ana wasichana na wao ndio wana wavulana au Tumewaumba Malaika kuwa wanawake nao wameshuhudia? Zindukeni! Hakika wao kwa uzushi wanasema: “Allaah amezaa.” Na hakika wao bila shaka ni waongo kwelikweli. Je, amechagua wasichana kuliko wavulana? Mna nini! Vipi mnahukumu? Je, hamkumbuki? Je, mna hoja za wazi? Basi leteni kitabu chenu mkiwa ni wakweli!” (37:149-157)

وَمَا مِنَّا إِلَّا لَهُ مَقَامٌ مَّعْلُومٌ وَإِنَّا لَنَحْنُ الصَّافُّونَ وَإِنَّا لَنَحْنُ الْمُسَبِّحُونَ

“Na hakuna miongoni mwetu isipokuwa ana mahali maalumu; na hakika sisi bila shaka tutajipanga safu na hakika sisi bila shaka ni wenye kumsabihi.” (37:164-166)

Miongoni mwao ni Jibriyl (´alayhis-Salaam). Kazi yake ni kupeleka Wahy. Amesema (Ta´ala):

قُلْ مَن كَانَ عَدُوًّا لِّجِبْرِيلَ فَإِنَّهُ نَزَّلَهُ عَلَىٰ قَلْبِكَ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Sema: “Yeyote aliyekuwa adui wa Jibriyl, basi hakika yeye ameiteremsha Qur-aan katika moyo wako kwa idhini ya Allaah.” (02:97)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona juu na akiwa na mbawa zake mia sita na umbile lake kubwa limefunika upeo wa juu. Kisha baada ya hapo akamuona mbinguni usiku wa safari ya mbinguni. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ

“Na kwa hakika amemuona katika uteremko mwingine. Kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa. Karibu yake ndio ipo bustani inayokaliwa.” (53:13-15)

Hakumuona katika umbile lake isipokuwa mara mbili hizi tu. Kuhusiana na mara nyinginezo, alijionyesha katika muonekano wa mtu na mara nyingine katika muonekano wa Dihyah al-Kalbiy. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Jibriyl:

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ مُطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ وَمَا صَاحِبُكُم بِمَجْنُونٍ وَلَقَدْ رَآهُ بِالْأُفُقِ الْمُبِينِ

“Hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu, Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye ´Arshi, anayetiiwa, tena muaminifu! Na wala huyu mwenzenu hana wazimu – na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho uliosafi.” (81:19-23)

Malaika mwingine ni Mikaaiyl. Kazi yake ni mazao na namna yatakavyogawiwa. Yote hayo yanatokamana na maamrisho ya Allaah (´Azza wa Jall). Imaam Ahmad amepokea kutoka kwa Anas ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Jibriyl:

“Ni kwa nini sijapatapo kumuona Mikaaiyl akicheka?” Akasema: “Mikaaiyl hajapatapo kucheka tangu uumbwe Moto.”

Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Mikaaiyl:

مَن كَانَ عَدُوًّا لِّلَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَرُسُلِهِ وَجِبْرِيلَ وَمِيكَالَ فَإِنَّ اللَّـهَ عَدُوٌّ لِّلْكَافِرِينَ

“Yeyote aliyekuwa adui wa Allaah na Malaika Wake, na Mitume Yake, na Jibriyl, na Miykaal, basi hakika Allaah ni adui kwa makafiri.” (02:98)

Miongoni mwao kuna mwingine ambaye ni Israafiyl. Kazi yake ni kupuliza baragumu ambalo atalipuliza mara tatu baada ya kuamrishwa na Mola Wake (´Azza wa Jall); mara ya kwanza itakuwa ya mfazaiko, ya pili ya kufa na ya tatu kwa ajili ya kusimama kwa ajili ya Mola wa walimwengu. Malaika watatu hawa ndio wale waliotajwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika du´aa yake ya swalah ya usiku:

“Ee Allaah! Mola wa Jibraaiyl, Mikaaiyl na Israafiyl. Muumba wa mbingu na ardhi. Mjuzi wa yenye kujificha na yenye kuonekana. Hakika Wewe utahukumu baina ya waja Wako katika yale yote waliyotofautiana. Niongoze katika yale yaliyotofautiana kwayo kwa idhini Yako – kwani hakika Wewe unamuongoza Umtakaye katika njia iliyonyooka.”

Imepokelewa na Muslim.

Katika “Sunan” ya an-Nasaa´iy imepokelewa kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Mola wa Jibraaiyl, Mikaaiyl na Israafiyl. Ninajilinda Kwako kutokamana na vuke la Moto na adhabu ya kaburi.”

Kadhalika kuna Malaika wa mauti. Kazi yake ni kutoa roho. Amesema (Ta´ala):

قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ

“Sema: “Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu kisha kwa Mola wenu mtarejeshwa.”” (32:11)

Vilevile kuna Malaika ambao kazi yao wamewekwa ili kumhifadhi mwanadamu katika hali zake zote; katika ukazi wake, anapokuwa safarini, anapokuwa amelala na anapokuwa macho. Amesema (Ta´la):

سَوَاءٌ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ

“Ni mamoja kwenu anayefanya siri kauli yake au anayeisema kwa juu na anayenyemelea usiku na anayetembea huru mchana. Ana [Malaika] wanaofuatana mfululizo mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa amri ya Allaah. Hakika Allaah habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. Na Allaah akiwatakia watu uovu basi hakuna wa kuurudisha. Na wala hawana mlinzi yeyote badala Yake ” (13:10-11)

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amefasiri maneno Yake (Ta´ala) “Ana wanaofuatana mfululizo” ifuatavyo:

“Ni Malaika wenye kumlinda mbele yake na nyuma yake. Pindi wakati wake wa kueshi unapokwisha, basi wanajitenga naye.”

Malaika wengine ni waandishi Watukufu. Ni wale wenye kuandika matendo mema na maovu ya waja. Amesema (Ta´ala):

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ كِرَامًا كَاتِبِينَ يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ

“Na hakika juu yenu bila shaka mmewekewa wenye kulinda, watukufu wanaoandika, wanajua yale myafanyayo.” (82:10-12)

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nyumba yenye kuamiriwa mbinguni wanaingia – na katika upokezi mwingine “wanaswali” – kila siku Malaika elfu sabini na baada ya hapo hawarejei tena.”

Yule mwenye kupinga kuwepo kwa Malaika ni kafiri kwa mujibu wa maafikiano ya waislamu. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا

“Na atakayemkufuru Allaah na Malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Yake na siku ya Mwisho, basi kwa hakika amepotoka upotofu wa mbali.” (04:136)

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 31-39
  • Imechapishwa: 21/06/2020