03. Uwajibu wa kuogopa na kujifunza vitenguzi vya Uislamu

Uislamu una mambo yanayoutengua. Mtu anaweza kuingia katika Uislamu, lakini hata hivyo akafanya vitu ambavyo vikamtoa katika Uislamu na huku akawa anajua au hajui. Kwa hivyo ni wajibu kwa mtu kujua vitenguzi hivi.

Mtume Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) alichelea shirki juu ya nafsi yake. Pamoja na kuwa yeye ndiye aliyeyavunja masanamu na akaudhiwa kwa ajili ya Allaah. Lakini pamoja na haya yote hakuiaminisha nafsi yake na akasema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ

“Uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu. Mola wangu! Hakika hao wamepoteza wengi sana katika watu.” (Ibraahiym 14:35)

Pindi alipoona wingi wa shirki na wengi waliopewa mtihani, ndipo akachelea juu ya nafsi yake. Mtu ni mtu. Isitoshe wale waliotumbukia katika shirki ni watu. Mtu asiitakase nafsi yake na wala asijiaminishe na dini yake. Kinyume chake anatakiwa kuwa na khofu juu ya dini yake zaidi kuliko anavyoichelea nafsi, mali na heshima yake:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ

“Uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu. Mola wangu! Hakika hao wamepoteza wengi sana katika watu.” (Ibraahiym 14:35)

Maudhui haya – mambo yanayotengua Uislamu – wanachuoni waliyatilia umuhimu tangu hapo zamani mpaka hivi sasa. Mambo yanatakiwa kuwa hivo. Walitunga vitabu vya kipekee na wakaiwekea mlango katika vitabu vya Fiqh wakiipa jina “Mlango: Hukumu ya mwenye kuritadi” ambapo ndani ya mlango huu wakataja vitenguzi vya Uislamu na hukumu ya yule anayetumbukia katika kitu katika hayo. Wametaja vitenguzi aina nyingi ambavyo huenda hata mtu asivifikirie. Lakini hata hivyo (Rahimahumu Allaah) wakavidhibiti na kuvibainisha na pia wakabainisha hukumu ya ambaye ametumbukia katika kitu katika hayo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 17
  • Imechapishwa: 07/02/2017