03. Ulazima wa Sunnah juu ya kuifahamu Qur-aan na mfano wa hayo

Amesema (Ta´ala):

وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا

“Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke wakateni mikono yao.” (05:38)

Huu ni mfano mzuri juu ya hilo. Kuiba kumetajwa kwa kuachiliwa kama ilivyo mkono. Hivyo Sunnah ya kimaneno ikaja kubainisha na ikafungamanisha na mwizi anayeiba robo ya dinari. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msiukate mkono isipokuwa kwa [yule mwenye kuiba] robo ya dinari na zaidi ya hapo.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ameibainisha vilevile kwa njia nyingine ambayo ni kwa kitendo chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au matendo ya Maswahabah wake na akawakubalia. Walikuwa wakikata mikono ya wezi, kama inavyotambulika kupitia vitabu vya Hadiyth na Sunnah ya kimaneno ikaja kubainisha ni upi mkono uliokusudiwa katika Aayah ya Tayammum:

فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ

“Futeni nyuso zenu na mikono yenu.”[1]

ya kwamba ni kitanga cha mkono. Vilevile amebainisha kwa kusema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tayammum inakuwa kwa kupiga usoni na kwenye vitanga vya mikono.”

Ameipokea Ahmad, al-Bukhaariy na Muslim na wengineo kupitia kwa ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Chukua baadhi ya Aayah nyingine ambazo hazikuweza kufahamika ufahamu sahihi vile alivyokusudia Allaah (Ta´ala) isipokuwa kupitia Sunnah.

1- Amesema (Ta´ala):

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ

“Wale walioamini na hawakuchanganya imani zao na dhulma, hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.” (06:82)

Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walielewa maneno Yake:

بِظُلْمٍ

“… na dhulma… “

juu ya ujumla wake unaokusanya dhuluma zote ikiwa ni pamoja vilevile na dhuluma ndogo. Kwa ajili hiyo ndio maana Aayah ikawatatiza na wakamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni nani kati yao ambaye hajaichanganya imani yake na dhuluma. Akawajibu kwa kuwaambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Sio hiyo. Bali hiyo ni shirki. Je, hamkusikia maneno ya Luqmaan:

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhulma kubwa mno”? (72:13)

Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo.

2- Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَقْصُرُوا مِنَ الصَّلَاةِ إِنْ خِفْتُمْ أَن يَفْتِنَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا

“Mtakaposafiri katika ardhi basi si dhambi kwenu kufupisha swalah mkikhofu kwamba waliokufuru watakushambulieni.” (04:101)

Udhahiri wa Aayah hii unapelekea ya kwamba kufupisha swalah safarini kumeshurutishwa kupatikane khofu. Kwa ajili hiyo baadhi ya Maswahabah walimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwa nini wanafupisha swalah ilihali wako katika amani ambapo akawajibu: “Ni swadaqah ya Allaah ambayo Allaah amekutunukieni. Hivyo ipokeeni swadaqah Yake.”

Ameipokea Muslim.

3- Amesema (Ta´ala):

حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ

“Mmeharamishiwa nyamafu na damu… “ (05:03)

Sunnah ya kimaneno ikabainisha kuwa nyamafu ya nzige, samaki, ini na wengu katika damu ni halali. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tumehalalishiwa nyamafu mbili na damu mbili; nzige na samaki aina zote, ini na wengu.”

Ameipokea al-Bayhaqiy na wengineo kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka kwa Swahabah. Mlolongo wa wapokezi unaotoka kwa Swahabah ni Swahiyh na uko katika hukumu ya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuwa jambo hili halisemwi kutokamana na maoni.

4- Amesema (Ta´ala):

قُل لَّا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ أَوْ فِسْقًا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ

“Sema: “Sipati katika yale niliyofunuliwa Wahy kwangu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni najisi au ufasiki kimetajiwa asiyekuwa Allaah.” (06:145)

Sunnah ikaja kuharamisha mambo ambayo hayakutajwa katika Aayah hii. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kila mnyama wa mwitu mwenye kutia meno na kila ndege mwenye kutumia makucha ni haramu.”

Katika mlango huu kuna Hadiyth zengine zinazokataza hilo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Khaybar:

“Allaah na Mtume wake wamekukatazeni [kula] nyama ya punda, kwani hakika ni uchafu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

5- Amesema (Ta´ala):

قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ

“Sema: “Nani aliyeharamisha mapambo ya Allaah ambayo amewatolea waja Wake na vile vizuri katika riziki?” (07:32)

Sunnah nayo ikaja kubainisha ya kwamba kuna katika mapambo ambayo ni haramu. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa siku moja aliwatokea Maswahabah wake na katika mkono wao mmoja walikuwa na hariri na katika mkono mwingine walikuwa na dhahabu ambapo akawaambia:

“Viwili hivi ni haramu kwa wanaume na ni halali kwa wanawake.”

Ameipokea al-Haakim na ameisahihisha. Hadiyth zilizo na maana hiyo ni nyingi na zinajulikana katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na ya Muslim na kwenginepo.

Kuna mifano mingine mingi inayojulikana kwa wanachuoni watambuzi wa Hadiyth na Fiqh.

[1] 04:43 na 05:06

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manzilat-us-Sunnah fiyl-Islaam, uk. 7-10
  • Imechapishwa: 10/02/2017