03. Ujuzi juu ya Allaah, Mtume Wake (صلى الله عليه وسلم) na Uislamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la kwanza: Ujuzi, nao ni ujuzi wa kumjua Allaah, ujuzi wa kumjua Mtume Wake na ujuzi wa kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili.

MAELEZO

Ujuzi – Nao ni ule ujuzi wa kumjua Allaah (´Azza wa Jall) kwa moyo kwa njia ambayo italazimisha mtu kuyakubali yale aliyoweka katika Shari´ah, kujisalimsiha nayo na kuyanyenyekea na kuhukumu kwa mujibu wa Shari´ah Yake ambayo imekuja na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mja atamjua Mola Wake kwa kutazama ujumbe wa Shari´ah ndani ya Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jalla) na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja vilevile na kutazama alama za kilimwengu ambazo ni viumbe. Kwani mtu kila pale atapotazama ishara hizi, basi huongezeka ujuzi wake juu ya Mola Wake na Yule anayemwabudu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ وَفِي أَنفُسِكُمْ ۚ أَفَلَا تُبْصِرُونَ

”Katika ardhi zipo alama kwa wale wenye yakini na katika nafsi zenu. Kwa nini hamuoni?” (adh-Dhaariyaat 51 : 20-21)

Ujuzi wa kumjua Mtume Wake – Nao ni ujuzi wa kumjua Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa utambuzi ambao utalazimisha kukubali uongofu na dini ya haki aliyokuja nayo, kumsadikisha kwa yale aliyoelezea, kutekeleza amri yake kwa yale aliyoamrisha, kujiepusha na yale aliyokataza na kuyagombeza, kuhukumu kwa Shari´ah yake na kuridhika na hukumu yake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Sivyo hivyo, naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana baina yao kisha wasione katika nyoyo zao uzito wowote katika yale uliyohukumu na wajisalimishe ukweli wa kujisalimisha.” (an-Nisaa´ 04 : 65)

إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

”Hakika neno la waumini wanapoitwa kwa Allaah na Mtume Wake ili awahakumu baina yao, husema: “Tumesikia na tumetii”; na hao ndio wenye kufaulu.” (an-Nuur 24 : 51)

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana katika jambo lolote basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa kweli mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni njia bora na matokeo mazuri zaidi.” (an-Nisaa´ 04 : 59)

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake; isije kuwasibu fitina au ikawasibu adhabu iumizayo.” (an-Nuur 24 : 63)

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Unajua fitina ni kitu gani? Fitina ni shirki. Huenda ataporudisha kitu katika maneno yake akaingiwa moyoni mwake na kitu katika upotevu na hivvyo akaangamia.”

Kuijua dini ya Kiislamu – Uislamu, kwa maana yake iliyoenea, ni kumwabudu Allaah kwa yale aliyoweka katika Shari´ah tangu pale alipotumiliza Mitume mpaka pale Qiyaamah kitaposimama. Hili Allaah (´Azza wa Jall) amelitaja katika Aayah nyingi ambazo zinajulisha kwamba Shari´ah zote zilizotangulia zilikuwa zimejengeka juu ya kujisalimisha kwa Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Ta´ala) Amesema kuhusu Ibraahiym:

رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ

“Mola wetu, Tujaalie tuwe wenye kujisalimisha Kwako pamoja na kizazi chetu wawe ummah wenye kujisalimisha Kwako.” (al-Baqarah 02 : 128)

Kuhusu Uislamu kwa maana maalum baada ya kutumilizwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), inakuwa ni maalum kwa yale aliyotumilizwa kwayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yale aliyotumwa nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yamefuta dini zote zilizotangulia na kwa ajili hiyo ikawa yule anayemfuata ndio muislamu na asiyemfuata hawi muislamu. Kwa njia hiyo wafuasi wote wa Mitume ni waislamu katika zama za Mitume wao. Mayahudi walikuwa ni waislamu katika zama za Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakristo pia walikuwa ni waislamu katika zama za ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini pale alipotumilizwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakamkufuru na hivyo wakazingatiwa sio waislamu.

Dini hii ya Kiislamu ndio dini pekee yenye kukubaliwa mbele ya Allaah na itakayomnufaisha yule anayeifuata. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

”Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.” (Aal ´Imraan 03 : 19)

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

”Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu, basi haitokubaliwa kutoka kwake, naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (Aal ´Imraan 03 : 85)

Uislamu huu ndio ule Uislamu ambao Allaah amemtukuza nao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Ummah wake. Allaah (Ta´ala) Amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo hii Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (al-Maaidah 05 : 03)

Kwa dalili – Dalili ni kile kinachoelekeza katika malengo. Dalili zinazoelekeza katika hilo ni za Qur-aan na Sunnah na za kiakili. Dalili za Qur-aan na Sunnah ni zile zilizothibiti kwa Wahy. Dalili za kiakili ni zile zilizothibiti kwa kufikiria na kuzingatia. Allaah (´Azza wa Jall) ametaja kwa wingi aina hii ndani ya Kitabu Chake. Ni Aayah ngapi Allaah ametaja kwamba miongoni mwa alama Zake ni kadhaa na kadhaa? Namna hii ndivo zinavyothibitishwa dalili za kiakili zinazojulisha juu ya uwepo wa Allah (Ta´ala).

Kuhusu kumjua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa dalili za Qur-aan na Sunnah, mfano wake ni maneno Yake (Ta´ala):

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah.” (al-Fath 48 : 29)

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ

“Muhammad si yeyote isipokuwa ni Mtume tu; wamekwishapita kabla yake Mitume.” (Aal ´Imraan 03 : 144)

Wakati huohuo mtu akajisaidia kwa dalili za kiakili na kufanya utafiti na kuzingatia ule ujumbe wa wazi aliokuja nao. Kubwa zaidi katika hizo ni Kitabu cha Allaah (´Azz wa Jall) ambacho ndani yake mna maelezo mengi ya kweli na yenye manufaa na hukumu zenye kutengeneza na ambazo ni adilifu. Nyenginezo ni ile miujiza aliyofanya, mambo yenye kufichikana aliyoelezea ambayo hayawezi kujulikana isipokuwa kwa njia ya Wahy na ambayo yalitokea kama alivyoelezea.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 15/05/2020