03. Ujumbe wa Mtume unabainisha haki katika misingi na matawi ya dini

Ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) una mambo mawili:

1- Elimu yenye manufaa.

2- Matendo mema. Allaah (Ta´ala) amesema:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَى وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ

“Yeye ndiye Aliyemtuma Mtume Wake kwa mwongozo na dini ya haki ili aidhihirishe ishinde dini zote japo watachukia washirikina.”[1]

Mwongozo ni elimu yenye manufaa na dini ya haki ni matendo mema yanayofanywa kwa ajili ya Allaah pekee kutokana na Shari´ah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Elimu yenye manufaa ni kila elimu ambayo inaunufaisha Ummah hapa duniani na Aakhirah. Kitu cha kwanza kinachoingia katika elimu hiyo yenye manufaa ni kuwa na elimu juu ya majina, sifa na matendo ya Allaah. Elimu hii ndio elimu yenye manufaa zaidi katika ujumbe wa kiungu na katika Da´wah ya kinabii. Kwayo ndio kuna kusimama kwa dini kimaneno, kimatendo na kiimani.

Kutokana na sababu hiyo ikawa ni jambo lisilowezekana kabisa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaipuuza elimu hii na asiibainishe kwa njia bainifu na ilio ya wazi yenye kuondosha shaka na utata. Ni jambo lisilowezekana kabisa kutokana na sababu zifuatazo:

1- Ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulikuwa na nuru na mwongozo. Allaah amemtuma akiwa ni mwenye kutoa bishara njema na mwenye kuonya. Alilingania katika dini ya Allaah kwa idhini Yake na alikuwa ni taa lenye kuangaza. Alifikisha mpaka akaucha Ummah wake katika njia ya wazi kabisa usiku wake ni kama mchana wake. Hakuna mwenye kupinda na njia hii isipokuwa anayestahiki maangamivu. Mwangaza ulio mkubwa na wa wazi kabisa ambao moyo unaweza kufikia ni kuwa na utambuzi juu ya majina, sifa na matendo ya Allaah. Hivyo ni lazima iwe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilibainisha hili kwa njia iliokuwa bora kabisa.

2- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliubainishia Ummah wake yale yote wanayohitajia katika maisha haya na Aakhirah. Aliwafunza mpaka adabu za kula, adabu za kunywa, adabu za kukaa, adabu za kulala na mfano wa hayo. Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekufa na hakuna ndege anayeruka kwa mbawa zake hewani, isipokuwa ametutajia elimu fulani juu yake.”

Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote ya kwamba kuwa na elimu juu ya Allaah na majina Yake, sifa na matendo Yake ni jambo linaloingia ndani ya sentesi hii iliyoenea. Bali uhakika wa mambo ni kwamba ndio jambo la kwanza linaloingia humo kutokana na haja kubwa ya jambo hilo.

3- Kumuamini Allaah (Ta´ala) na majina, sifa na matendo Yake ndio msingi wa dini na Da´wah ya Mitume. Ndio wajibu mkubwa na ulio bora zaidi ambao moyo unaweza kuufikia na ambao akili inaweza kuuelewa. Ni vipi basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaweza kuipuuza elimu hii pasi na kuifunza na kuibainisha ilihali alikuwa akifundisha mambo ambayo hayakuwa ni yenye umuhimu na ubora mkubwa sawa na hayo?

4- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ndiye kiumbe mjuzi zaidi kumtambua Mola Wake. Alikuwa ni mwenye kupenda kutoa nasaha na mwenye ufaswaha mkubwa zaidi. Kujengea juu ya mambo haya ambayo yanapelekea katika ubainifu ulio mkamilifu zaidi, ni jambo lisilowezekana akaacha kubainisha maudhui ya kumuamini Allaah na majina Yake, sifa na matendo Yake yakawa ni yenye kutatiza na yasiyokuwa wazi.

5- Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ni lazima wazungumze haki katika suala hili. Vinginevyo ima watanyamaza au watazungumza batili. Yote mawili hayawezekani kwao:

Endapo watanyamaza, watanyamaza ima kwa sababu ni wajinga juu ya yale majina na sifa ambazo ni wajibu kwa Allaah (Ta´ala) awe nazo, ambazo inafaa kuwa nazo na ambazo haifai kuwa nazo, au wawe wamenyamaza kwa sababu ya kuificha elimu hii. Yote mawili hayawezekani.

Kuhusu uwezekano wa ujinga, ni jambo lisilowezekana kwa moyo wowote ulio na uhai na uelewa, utashi wa elimu na pupa ya ´ibaadah kutofanya utafiti juu ya kumuamini Allaah (Ta´ala) na kuwa na utambuzi wa majina na sifa Zake na kuhakikisha hilo kwa ujuzi na kiimani. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba zile karne bora, ambapo wabora wao ni Maswahabah, ndio watu wenye mioyo ilio na uhai zaidi, kupenda zaidi kheri na kuihakiki elimu yenye manufaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu bora ni karne yangu. Kisha wale watakaofuata. Kisha wale watakaofuata.”[2]

Ubora wao huu unajumuisha maneno, matendo na ´Aqiydah inayowakurubisha kwa Allaah.

Lau tutasema kuwa walikuwa ni wajinga juu ya suala hili, karne zilizokuja baada yao ni zenye kustahiki ujinga huu zaidi. Kwa sababu njia ya kipekee ya kujua ni majina yepi na sifa ambazo anatakiwa kuthibitishiwa au kutothibitishiwa Allaah (Ta´ala) ni kupitia Ujumbe. Maswahabah ndio wakati kati baina ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Ummah. Kujengea juu ya hili, itapelekea kutokuwepo yeyote ambaye ana ujuzi kuhusu mada hii, jambo ambalo haliwezekani.

Vilevile ni jambo lisilowezekana wakawa wameficha elimu. Hakuna mtu mwerevu na mwadilifu ambaye anajua hali za Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na jinsi walivyokuwa na pupa ya kueneza na kuwafikishia Ummah elimu yenye manufaa na halafu aseme kuwa walificha haki na khaswa katika jambo muhimu kabisa, nalo si jengine ni elimu ya kumtambua Allaah na majina na Sifa Zake. Isitoshe kumepokelewa sehemu kubwa kutoka kwao juu ya maudhui haya. Anayajua kila yule mwenye kuyafuatilia.

Kadhalika ni jambo lisilowezekana wakawa wamezungumza batili. Hilo ni kwa njia mbili:

1- Batili haiwezi kujengwa juu ya dalili sahihi na ni jambo lenye kujulikana kuwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa ni watu wako mbali kabisa kuzungumzia kitu ambacho hakikujengwa juu ya dalili sahihi na khaswa juu ya suala lenye kuhusu kumuamini Allaah (Ta´ala) na mambo yaliyofichikana. Walikuwa wamakinifu zaidi kujisalimisha na maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَلا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ

“Na wala usiyafuate yale usiyokuwa nayo elimu.”[3]

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْأِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَنْ تُشْرِكُوا بِاللَّهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَاناً وَأَنْ تَقُولُوا عَلَى اللَّهِ مَا لا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika Mola wangu ameharamisha machafu – [sawa] yaliyodhihirika na yaliyofichika – na dhambi, ukandamizaji bila ya haki na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa [chochote kile] ambacho hakukiteremshia mamlaka na kusema juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[4]

2- Kuzungumza batili ima kunatokana na ujinga wa kutoijua haki au kwa kukusudia kuwapotosha viumbe. Yote mawili ni mambo yasiyowezekana inapokuja kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

Kuhusiana na uwezekano wa ujinga, tumeshatangulia kulibainisha.

Ama kuhusu uwezekano wa kutaka kuwapotosha viumbe, haya ni makusudio mabaya. Makusudio kama haya haiwezekani yakatoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ambao walikuwa ni wenye kujulikana kwa nasaha zao timilifu na kuupendelea kwao kheri Ummah. Lau ingelikuwa ni jambo lenye kuwezekana kuwa na makusudio mabaya katika jambo hili, basi kadhalika ingelikuwa pia wanaweza kuwa na makusudio mabaya katika mambo mengine yote ya elimu na dini. Kwa hali hiyo wangelikuwa sio waaminifu katika mambo yote. Hii ni batilifu kubwa kabisa kwa sababu inalazimisha Shari´ah nzima kutukanwa.

Pale itapobainika kuwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ni lazima wawe ni wenye kuzungumza haki katika suala hili, basi ima walifanya hilo kwa akili zao au kwa njia ya Wahy. Haiwezekani ikawa kwa akili zao kwa vile akili haiwezi kutambua kwa ufafanuzi ni sifa zepi kamilifu ambazo ni wajibu kwa Allaah (Ta´ala) kusifika nazo. Hivyo ni lazima iwe hilo chaguo la pili, nalo ni kwamba waliipokea elimu hii kupitia Ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hilo linalazimisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibainisha haki katika majina na sifa za Allaah, na hili ndilo linalotakikana.

[1] 09:33

[2] al-Bukhaariy (2652) na Muslim (2533).

[3] 17:36

[4] 07:33

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 09-11
  • Imechapishwa: 06/01/2020