Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa kwanza:

Kumtakasia dini Allaah (Ta´ala), hali ya kuwa pekee hana mshirika na kubainisha kinyume chake ambacho ni kumshirikisha Allaah.

MAELEZO

Kumtakasia dini Allaah… – Kumtakasia dini Allaah maana yake ni kwamba mtu akusudie kwa ´ibaadah yake kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala) na kuingia Peponi. Hilo linapatikana kwa mtu awe ni mwenye kumtakasia nia Allaah; amtakasie nia Allaah katika mapenzi yake, amtakasie nia Allaah katika kumtukuza Kwake, amtakasie nia Allaah kwa uinje na kwa undani wake. Kwa msemo mwingine hakuna anachokusudia kwa ´ibaadah yake isipokuwa kutafuta kuona uso wa Allaah (Ta´ala) na kuingia Peponi. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

”Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika; na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni muislamu wa kwanza.”[1]

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ

“Rejeeni kwa Mola wenu na jisalimisheni Kwake.”[2]

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ

“Mungu wenu ni Mungu mmoja pekee; hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”[3]

فَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا

“Kwa hiyo mwabudiwa wenu wa haki ni Mungu Mmoja pekee, basi Kwake jisalimisheni!”[4]

Allaah amewatumiliza Mitume wote kwa kazi hiyo. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[5]

Allaah amelibainisha hilo ndani ya Kitabu Chake. Mtunzi wa kitabu amesema:

“… kwa njia mbalimbali kwa maneno yanayofahamika na wale wajinga kabisa katika watu.”

Ameibainisha vyema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amekuja (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuihakikisha Tawhiyd, kuitakasa na kuisafisha kutokamana na kila uchafu na kufunga kila njia inayoweza kumfikisha mtu kutokomeza au kuidhoofisha Tawhiyd hii. Kuna mtu mmoja alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Akitaka Allaah na ukataka wewe.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Je, umenifanya kuwa mshirika wa Allaah? Bali sema “Akitaka Allaah pekee.”[6]

Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkemea bwana huyu kuyaambatanisha matashi yake na matashi ya Allaah (Ta´ala) kwa herufi inayopelekea kusawazisha kati yao na akafanya jambo hilo ni kumfanyia Allaah wenza.

Miongoni mwa hayo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuapa kwa jina la mwingine asiyekuwa Allaah na akafanya jambo hilo ni katika shirki. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah basi amekufuru au ameshirikisha.”[7]

Hayo ni kwa sababu kuapa kwa jina la mwingine asiyekuwa Allaah ni kumtukuza yule mwapiwaji kwa ambayo hayastahiki mwengine asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Vilevile wakati alipojiwa na kikosi wakasema: “Ee mbora wetu na mtoto wa mbora wetu! Bwana wetu na mtoto wa bwana wetu.” Ndipo akasema: “Enyi watu! Semeni msemayo, au baadhi yake tu, na wala asikupotezeni shaytwaan. Mimi ni Muhammad, ni mja wa Allaah na Mtume Wake. Sipendi mnipandishe zaidi ya cheo changu alichonipa Allaah (´Azza wa Jalla).”[8]

Mtunzi (Rahimahu Allaah) ameweka mlango kuhusu hilo katika “Kitaab-ut-Tawhiyd” ambapo akaupa jina la: “Mtume (صلى الله عليه وسلم) kuihami Tawhiyd na kuziba njia zote za shirki”.

[1] 06:162-163

[2] 39:54

[3] 02:163

[4] 22:34

[5] 21:25

[6] al-Bukhaariy (783). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (139).

[7] Abu Daawuud (3251) na at-Tirmidhiy katika “Sunan” yake (1540). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (2787).

[8] al-Bukhaariy katika “al-Adaab-ul-Mufrad” (875). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika ”Swahiyh-ul-Adaab-ul-Mufrad”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 07-09
  • Imechapishwa: 16/06/2021