03. Salaf hawakuzifasiri sifa za Allaah


10- Wakati ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alipopata khabari kwamba Swabiygh anauliza juu ya mambo yasiyokuwa wazi, alimwandalia kuti la mti wa mtende. Wakati alipokuwa akikhutubu akasimama na kumuuliza:

وَالذَّارِيَاتِ ذَرْوًا فَالْحَامِلَاتِ وِقْرًا

“Ninaapa kwa pepo zinazotawanya; ninaapa kwa mawingu yanayobeba mzigo.”[1]

´Umar akashuka chini kutoka kwenye mimbari na kusema: “Unaitwa nani?” Akajibu: “Mimi ni mja wa Allaah Swabiygh.” ´Umar akasema: “Na mimi ni mja wa Allaah ´Umar. Funua kichwa chako.” Mtu yule akafunua kichwa chake ambapo akaona yuko na nywele. ´Umar akasema: “Lau ungelikuwa kipara basi ningekukata shingo yako.” Halafu akaamrisha achapwe vikali. Baada ya hapo akaamrisha atumwe Baswrah ambapo akaamrisha wakazi wa huko wasiketi naye. Alikuwa kama ngamia wa kushangaza; alikuwa haketi karibu na yeyote isipokuwa wanasema: “Kumbukeni amri ya kiongozi wa waumini!” Papohapo wanasimama na kumwacha peke yake. Hatimaye akatubu na kuapa kwa Allaah ya kwamba yamemtoka yale yote yaliyouwa kichwani mwake. Hapo ndipo ´Umar aliwaamrisha watu kukaa naye. Wakati Khawaarij walipojitokeza wakamwambia: “Huu ni wakati wako.” Akasema: “Hapana. Nilinufaika na mawaidha ya mja mwema.”[2]

11- Kuna mtu alikuja kwa Maalik bin Anas (Radhiya Allaahu ´anh) na akasema:

“Ee Abu ´Abdillaah!

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[3]

Amelingana vipi?”

Maalik akaanza kutokwa na kijasho ambapo wasikilizaji wanasubiri atasema nini. Halafu akamtazama na kusema:

“Kulingana kunajulikana. Namna haijulikani. Kuamini hilo ni wajibu na kuuliza juu ya hilo ni Bid´ah. Mimi sikuoni isipokuwa mtu muovu.”

Halafu akaamrisha atolewe nje.

12- Imepokelewa kutoka katika kundi kubwa katika wao ya kwamba wamesema kuwa haitakikani kwa mtu kupekua juu ya maudhui haya na kwamba sifa zinatakiwa kunukuliwa kama zilivyokuja. Maimamu wengi wamesema kuwa mfumo wao ni ule ambao hivi punde nimetoka kuutaja.

13- Shaykh Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Ahmad bin an-Naquur ametukhabarisha: Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy bin al-Husayn at-Twuraythiythiy ametuhadithia: Abul-Qaasim Hibatullaah bin al-Hasan at-Twabariy ametuhadithia: Ahmad bin Muhammad bin Hafsw ametuhadithia: Ahmad bin Muhammad bin Maslamah ametuhadithia: Sahl bin ´Uthmaan bin Sahl ametuhadithia: Nilimsikia Ibraahiym bin al-Muhtadiy akisema: Nilimsikia Daawuud bin Twalhah akisema: Nilimsikia ´Abdullaah bin Abiy Haniyfah ad-Dawsiy akisema: Nilimsikia Muhammad bin al-Hasan akisema:

“Wanachuoni wote mashariki na magharibi wamekubaliana juu ya kwamba Qur-aan na Sunnah zilizonukuliwa na wapokezi waaminifu kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu sifa za Mola (´Azza wa Jall) zinatakiwa kuaminiwa pasi na kuzifasiri, kuzieleza wala kuzishabihisha. Mwenye kufasiri chochote katika hayo basi ametoka katika yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na amefarikiana na mkusanyiko. Hawakueleza na wala hawakufasiri. Waliamini kile kilichomo katika Qur-aan na Sunnah kisha wakanyamaza. Mwenye kusema kama alivosema Jahm amefarikiana na mkusanyiko. Kwa sababu amemweleza kama si kitu.”

14- Muhammad bin al-Hasan amesema kuhusiana na Hadiyth:

“Allaah hushuka katika mbingu ya dunia.”

“Hadiyth hizi zimepokelewa na watu waaminifu. Sisi tunazipokea, tunaziamini na wala hatuzifasiri.”[4]

[1] 51:01-02

[2] Tazama ”ash-Shariy´ah”, uk. 74, ya al-Aajurriy na ”´Aqiydat-us-Salaf”, uk. 83-85, ya as-Swaabuuniy.

[3] 20:05

[4] al-Laalakaa’iy (2/433).

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta'wiyl, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 29/04/2018