03. Sababu ya mwanadamu kupewa kila kitu

Amemuumba Aadam (´alayhis-Salaam) kutoka katika patupu, ambaye ndiye baba wa watu, kutokana na udongo na akamtia sura na akamuumba katika umbile zuri kabisa. Amesema (Ta´ala):

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ

”Hakika Tumemuumba mtu katika umbile bora kabisa.”[1]

Akamtunuku usikizi, uoni na akamtofautisha na viumbe wote kutokana na akili hii ambayo anapambanua kwayo kati ya kitu chenye kudhuru na chenye kunufaisha, kizuri na kibaya, cha kheri na shari. Hii ni sifa maalum ya mtu, kwa sababu Allaah amemtukuza. Amesema (Ta´ala):

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ

”Hakika Tumemuumba mtu katika umbile bora kabisa.”

يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ

“Ee mwanadamu! Nini kilichokughuri juu ya Mola wako mkarimu? Ambaye amekuumba akakusawazisha na akakupima na kukulinganisha sawa. Katika sura aliyotaka akakutengeneza.”[2]

Ni lazima kwa mtu huyu kumhimidi Allaah juu ya neema hii, kuishukuru na kutekeleza ile ´ibaadah ambayo Allaah (´Azza wa Jall) amemuwajibishia. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ

“Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. Sitaki kutoka kwao riziki yoyote na wala Sitaki wanilishe. Hakika Allaah ndiye Mwingi wa kuruzuku, Mwenye nguvu madhubuti.”[3]

Hivi kweli Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anayo haja ya ´ibaadah? Hana haja ya ´ibaadah. Mja ndiye ambaye anayo haja ya ´ibaadah ili apate kuwasiliana na Allaah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yeye ni mkwasi wa viumbe. Lau wote watakufuru hakuna chochote kitachopunguka katika ufalme Wake, na lau wote watamtii hakuna chochote kitachoogezeka katika ufalme Wake. Madhara au manufaa yanarejea kwao wenyewe. Amewaamrisha ´ibaadah ili apate kuwakirimu kwa jambo hilo na ili wapate kuwasiliana Naye (Subhaanahu wa Ta´ala). Vinginevyo iwapo wote wangelikufuru basi kusingemdhuru Allaah chochote:

وَقَالَ مُوسَىٰ إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ

“Muusa akasema: “Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah ni mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[4]

Lau wote wangelikuwa wema basi hakuna chochote kingeongeza katika ufalme Wake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema katika Hadiyth-ul-Qudsiy:

“Enyi waja wangu! Lau wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, watu wenu na majini wenu, wangekusanyika kwenye moyo wa mtu mchaji zaidi kati yenu, basi hayo yasingezidisha katika ufalme Wangu chochote. Enyi waja wangu! Lau wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, watu wenu na majini wenu, wangekusanyika kwenye moyo wa mtu muovu zaidi kati yenu, basi hayo yasingepunguza katika ufalme Wangu chochote.”[5]

Miongoni mwa neema za Allaah juu ya mtu huyu ni kwamba amemuumba katika umbile bora kabisa na akamuwepesishia vyote vilivyoko mbinguni na ardhini. Hivi vyombo vya safari na vyombo vya mawasiliano vyote hivi ni kwa ajili ya kumtumikia mwanadamu huyu, sio kwa ajili apetuke mpaka kwavyo, afanye kwavyo jeuri, kiburi na kuvitumia kuangamiza utu, malengo ni vimsaidie kumtii Allaah na kuwanufaisha viumbe Wake. Haijuzu kwa mtu kutengeneza uvumbuzi wa kuangamiza na silaha zinazowaangamiza watu. Vifaa hivi vinatakiwa kutumika kusaidia ulimwengu na kunufaisha watu wake.

[1] 95:4

[2] 82:6-8

[3] 51:56-58

[4] 14:08

[5] Muslim (2577).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 11-13
  • Imechapishwa: 29/06/2021