03. Mke mwema uhusiano wake na Allaah

Kitu cha kwanza nitachoanza nacho kutokana na yaliyotajwa kuhusu sifa za mke mwema katika Suurat an-Nisaa´:

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“Wanawake  wema  watiifu [kwa Allaah] na ni wenye kujihifadhi [kwa wengine] katika hali ya kutokuwepo waume zao kwa yale Allaah amewahifadhi.”[1]

Katika sehemu hii ya Aayah Allaah ameleta maelezo yaliyoenea na sifa zote tukufu za mwanamke mwema anazotakiwa kuwa nazo. Andiko hili tukufu linatufahamisha kwamba mke mwema ni yule aliyekusanya sifa mbili:

Sifa ya kwanza inahusiana na uhusiano wake kwa Mola Wake.

Sifa ya pili inahusiana na uhusiano wake kwa mume wake.

Uhusiano wake kwa Mola Wake unapatikana katika Kauli Yake (Subhaanah):

قَانِتَاتٌ

“… watiifu [kwa Allaah]… “

Ina maana ni mwenye kudumu katika kumtii Allaah, anahifadhi ´ibaadah na mtiifu kwa Allaah, anatilia umuhimu faradhi za Uislamu na kuacha kuyaapuza. Yote hayo yanaingia chini ya Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

قَانِتَاتٌ

“… watiifu [kwa Allaah]… “

Sehemu ya pili katika Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“… ni wenye kujihifadhi [kwa wengine] katika hali ya kutokuwepo waume zao kwa yale Allaah amewahifadhi.”

Ina maana anahifadhi haki za mume wake pindi anapokuwa hayupo na pindi anapoonekana. Anamhifadhi katika mali zake, kitandani na mambo yake ya wajibu:

حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“… ni wenye kujihifadhi [kwa wengine] katika hali ya kutokuwepo waume zao kwa yale Allaah amewahifadhi.”

Hata hivyo amefanikiwa kuihakiki sifa hii kwa sababu ya kule Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kumuwafiki. Yeye ndiye amemrahisishia. Ndio maana amesema:

حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“… ni wenye kujihifadhi [kwa wengine] katika hali ya kutokuwepo waume zao kwa yale Allaah amewahifadhi.”

Bi maana hawezi kufanikiwa kufanya hivo kwa sababu yeye ni mtu wa sawasawa, mwenye akili, busara na mwerevu, isipokuwa ni kutokana na uafikishaji wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kumrahisishia hilo. Hili linatukumbusha yale niliyotaja punde tu, nayo ni kwamba uzuri na wema ni kutokana na uafikishaji wa Allaah, usahilishaji Wake na msaada Wake.

Katika Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

قَانِتَاتٌ

“… watiifu [kwa Allaah]… “

kunaingia ndani yake mwanamke ambaye anahifadhi faradhi za Uislamu. Kuna Hadiyth nyingi ambazo zimepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na maana hii. Miongoni mwazo ni yale aliyopokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake[2] kupitia Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akiswali [swalah zake] tano, akafunga mwezi wake, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, ataingia mlango wowote wa Peponi autakao.”

Imaam Ahmad amepokea katika “al-Musnad” yake[3]  kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akiswali [swalah zake] tano, akafunga mwezi wake, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, ataambiwa: “Ingia Peponi kwenye mlango wowote wa Pepo uutakao.”

Tunampa hongera mwanamke wa Kiislamu kwa ahadi hii tukufu na fadhila kubwa na kheri ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amemuahidi nayo. Inahusiana na mambo mane tu ambayo anaweza kuyahesabu kwa kutumia vidole vya mkono wake mmoja na si vidole vya mikono yote miwili. Akiyahakikisha mambo haya mane ataambiwa siku ya Qiyaamah:

“Ingia Peponi kwa mlango wowote wa Pepo uutakao.”

Hivi kweli mwanamke ambaye anajitamania kheri juu ya nafsi yake si azitilie uzito na umuhimu sifa hizi na kuyadhibiti matendo haya? Anatakiwa kuhifadhi swalah zake, swawm zake, tupu na haki za mume wake ili aweze kushinda ahadi hii tukufu na fadhila na kheri hii kubwa ili aweze kuambiwa siku ya Qiyaamah:

“Ingia Peponi kwa mlango wowote wa Pepo uutakao.”

Msingi wa wema kwa mwanamke uko katika wema wake kwa Mola Wake kwa kumtii, kujikurubisha Kwake na kuzidhibiti ´ibaadah Zake kwa uzuri. Wema na msimamao huu ndio siri ya furaha yake, kufaulu kwake na mafanikio yake katika maisha yake yote kukiwemo na maisha yake ya kindoa, watoto wake kuwa wema na kizazi chake na kuishi kwake maisha ya baraka na mazuri.

Kwa ajili hiyo ndio maana ikawa ni jambo lililosisitizwa kwa yule mwenye kuitakia nafsi yake kheri na kwa wasimamizi ambao wanawatakia wasichana wao kheri kuwalea wanawake juu ya wema, msimamo, kuhifadhi ´ibaadah, faradhi za Uislamu na khaswa swalah tano na kufunga mwezi wa Ramadhaan na kujitenga mbali na mambo yote yanayoathiri utwaharifu wa mwanamke na utukufu wake. Ni hayo ndio yamebainishwa katika Hadiyth hii:

“… akahifadhi tupu yake… “

Mwanamke kuhifadhi tupu yake ni jambo linalohitajia kutoka kwake na kutoka kwa msimamizi wake kufunga milango na njia zote zinazopelekea katika ufisadi, shari na kusababisha madhambi. Hili ni jambo kubwa ambalo kwa kila yule mwenye kuitakia nafsi yake kheri anatakiwa kuilea nafsi yake juu ya hilo. Anatakiwa kuihifadhi nafsi yake daima katika kumtii Allaah, kumuabudu Allaah na kujikurubisha Kwake (Subhaaahu wa Ta´ala) kwa yale yanayomridhisha katika maneno mema na matendo mazuri. Jengine ni kwamba Allaah akimneemesha mume mzuri na wa kisawasawa, ni juu yake kumcha Allaah kwa kuhakikisha anazichunga haki za mume wake tokea ile siku ya kwanza ya ndoa.

Hili linawajibisha kukumbusha juu ya suala ambalo kosa lake limekuwa ni lenye kuenea na kusambaa. Nalo linahusiana na israfu na ubadhirifu unaokuwa katika usiku ule wa ndoa na katika matumizi ya ndoa. Hili ni jambo ambalo khatari yake ni kubwa na madhara yake ni makubwa. Wanawake wengi wanapotaka kuolewa wanachozingatia ni yale ya nje na wanawake wa rika sawa naye. Wanatazama ni nini walichofanya wanawake wengine katika ndoa mbalimbali. Wanafikiria kwa njia hiyo na hivyo kunakuwa israfu na ubadhirifu. Wanapoteza vingi na pesa nyingi zinaharibiwa katika visivyokuwa na maana. Aidha kunaweza kuwepo hata maovu na mambo ya haramu. Kwa ajili hiyo mwanzo huu unakuwa na utangulizi wa ndoa inakuwa ni sababu ya upungufu wa baraka na kheri.

Hali huwa sivyo ikiwa mwanamke na familia yake watajitenga mbali na hayo, kujiepusha na israfu, mambo ya maasi na madhambi na wakafanya matumizi kuwa rahisi na pasi na israfu wala ubadhirifu. Katika hali kunapatikana kheri na kufikiwa baraka. Imekuja katika Hadiyth Swahiyh katika “as-Sunan” ya Abu Daawuud[4] iliyopokelewa na ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Bora ya ndoa ni ile iliyo rahisi.”

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Wanawake walio na baraka zaidi ni wale ambao kuna urahisi zaidi kuwahudumikia.”[5]

Wanawake bora ni wale walio rahisi.

Kwa ajili hii ndio maana inatakikana kwa mwanamke na kwa wazazi wake wahakikishe ndoa iwe rahisi na isiwe na ugumu, unyenyekevu na sio majivuno, nzuri na yenye utulivu na kusiwe na israfu na ubadhirifu. Mambo yote haya yana taathira katika maisha yote ya ndoa kwa uzuri na ubaya.

Ikiwa ndoa ni rahisi na ikafanywa kuwa sahali na kujiepusha na mamabo ya israfu, hukabiliwa na baraka na kheri.

Kama ndoa itakuwa na israfu, ubadhirifu, maasi na aina mbalimbali ya madhambi, ni miongoni mwa sababu kubwa ya kukosekana baraka na tunaomba ulinzi kwa Allaah.

[1] 04:34

[2](3163).

[3] (1661).

[4] (2117). Ni Swahiyh kwa mujibu wa Imaam al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (1842).

[5] Ahmad katika “al-Musnad” (25120), an-Nasaa´iy katika “al-Kubraa” (9274) kupitia Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

 

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 12-19
  • Imechapishwa: 10/06/2017