03. Mizani ni Qur-aan na Sunnah


Ndugu msomaji nitakunakilia yale yaliyosemwa na baadhi ya wanazuoni katika masuala haya ili uwe juu ya ubainifu katika hayo. Wanazuoni (Rahimahumu Allaah) wameafikiana juu ya kwamba jambo la lazima ni kurudisha yale masuala ambayo watu wametofautiana kwayo katika Qur-aan na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yale yatayoamuliwa na kimoja wapo basi ndio Shari´ah inayolazimika kuifuata. Yanayokwenda kinyume navyo basi ni lazima kukitupa. Zile ´ibaadah ambazo hazikupokelewa kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah basi ni Bid´ah isiyojuzu kuitendea kazi sembuse kulingania na kuipa kuifadhilisha. Allaah (Subhaanah) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[1]

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

“Jambo lolote lile mlilokhitilafiana ndani yake, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[2]

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu.”[3]

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”[4]

Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hii.

Ni dalili za wazi zinazowajibisha kurudisha masuala ya makinzano katika Qur-aan na Sunnah na kuridhia kuhukumiwa navyo. Aidha hivo ndio muqtadha ya imani na kheri kwa waja duniani na Aakhirah.

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”

Bi maana mwisho mwema.

[1] 04:59

[2] 42:10

[3] 03:31-32

[4] 04:65

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 16/01/2022