03. Maulidi hayana chochote kuhusiana na Uislamu


Allaah (Subhaanah) amewakamilishia waja dini na akawatimizia neema Yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefikisha ufikishaji wa wazi. Hakuacha njia inamyomfikisha mtu Peponi na kumwepusha na Moto isipokuwa amewabainishia Ummah wake. Hayo yamethibiti katika Hadiyth Swahiyh kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah hajapatapo kumtuma Mtume yeyote isipokuwa ilikuwa ni haki juu yake kuuelekeza Ummah wake katika kheri anayoifahamu juu yao na kuwaonya na shari anayoifahamu juu yao.”[1]

Ameipokea Muslim katika ”as-Swahiyh” yake.

Ni jambo linalotambulika ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye bora ya Mitume na wa mwisho wao na ambaye amefikisha kwa kuenea zaidi na kuwatakia watu mema zaidi. Endapo kusherehekea mazazi ingelikuwa ni sehemu katika dini ambayo anairidhia Allaah (Subhaanah) basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angewabainishia Ummah wake, angeyafanya katika uhai wake au yangefanywa na Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum). Wakati hakukutokea chochote katika hayo basi ikapata kutambulika kwamba hayana chochote kuhusiana na Uislamu. Bali yanaingia miongoni mwa mambo yaliyozuliwa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameutahadharisha Ummah wake, kama tulivotangulia kuyataja katika Hadiyth mbili zilizotangulia. Zipo Hadiyth nyenginezo ambazo zimekuja zikiwa na maana hiyo kukiwemo maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Katika Khutbah ya ijumaa:

“Amma ba´d; hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa. Kila Bid´ah ni upotofu.”[2]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Zipo Aayah na Hadiyth nyingi kuhusu maudhui haya.

[1] Muslim (1844).

[2] Muslim (867).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 07-09
  • Imechapishwa: 11/01/2022