Hafungui mfungaji iwapo atatumia kitu kinachofunguza kwa kusahau, kutokujua au kwa kulazimishwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea.” (02:286)

إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ

”… isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu imani.” (16:106)

وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ

”Hapana dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini isipokuwa katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu.” (33:05)

Akisahau mwenye kufunga ambapo akawa amekula au akanywa, swawm yake haiharibiki. Kwa sababu amesahau.

Endapo atakula au atakunywa kwa kuamini kwamba jua limeshazama au alfajiri haijaingia, basi swawm yake haiharibiki. Kwa sababu hakujua.

Ikiwa atasukutua na maji yakaingia kooni mwake pasi na kukusudia, swawm yake haikuharibika. Kwa sababu hakufanya makusudi.

Akimwaga manii usingizini mwake swawm yake vilevile haiharibiki. Kwa sababu hakufanya kwa kukusudia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nubadh fiys-Swiyaam, uk. 03-04
  • Imechapishwa: 17/05/2018