03. Malengo ya maadui wa Uislamu juu ya mwanamke wa Kiislamu

Maadui wa Uislamu, bali naweza kusema maadui wa utu hii leo, miongoni mwa makafiri, wanafiki na wale ambao ndani ya mioyo yao mna maradhi ni wenye kukasirishwa na ile heshima na utukufu anaopata mwanamke wa Kiislamu ndani ya Uislamu. Kwa sababu lengo la maadui wa Uislamu katika makafiri na wanafiki wanataka mwanamke awe ni chombo cha kuangamizwa na kamba inayowavuta wale watu wenye imani dhaifu na watu wenye matamanio ya nguvu baada ya kuwashibiza wanawake matamanio yao. Amesema (Ta´ala):

وَيُرِيدُ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الشَّهَوَاتِ أَن تَمِيلُوا مَيْلًا عَظِيمًا

“Wale wanaofuata matamanio wanataka kukengeuka mkengeuko mkubwa mno.”[1]

Wale waislamu ambao ndani ya mioyo yao mna maradhi wanataka mwanamke awe ni bidhaa rahisi kwa wale wenye matamanio na wenye fikira na matamanio ya ki-Shaytwaan. Lengo lao wanamtaka mwanamke awe ni bidhaa iliowazi mbele ya macho yao ambapo watashareheka na urembo wa kumtazama au wanataka kufikia kwa mwanamke jambo ambalo ni baya zaidi kuliko hilo. Kwa ajili hiyo ndio maana utawaona wanaenda mbio kwelikweli kumtoa mwanamke nje ya nyumba yake ili aweze kushirikiana na wanaume katika kazi zao wakiwa bega kwa bega; wauguzi wa kike kuwahudumia wanaume hospitalini, wahudumu wa kike ndani ya ndege, mwalimu wa kike kwenye klasi ambayo ina mchanganyiko, muigizaji wa kike kwenye maigizo, mwimbaji wa kike au mtangazaji katika vyombo vya mawasiliano vya mchanganyiko hali ya kuwa uso wazi na mwenye kutia watu mtihani kwa sauti na sura yake. Magazeti ya uchiuchi yamemfanya mwanamke katika picha za wasichana, wenye kutia fitina na walio uchiuchi kuwa ni njia moja wapo ya kutangaza magazeti yao na kuyafanya yatoke. Baadhi ya wafanyabiashara na baadhi ya viwanda pia yamezifanya picha hizi kuwa ni njia ya kutangaza bidhaa zao. Wameziweka picha hizi juu ya zile biashara zao na vitu vyao wanavyovitangaza. Kwa sababu ya vitendo hivi vya kimakosa mwanamke ameiacha kazi yake ya kikweli nyumbani, jambo ambalo limewalazimu waume zao kuwaleta wafanyakazi wa kike wa kigeni ili kuwalelea watoto wao na kuwapangia mambo ya nyumba zao. Mambo hayo kwa kiasi kikubwa yamepelekea katika fitina na maovu mengi.

Sisi hatumkatazi mwanamke kufanya kazi nje ya nyumba yake ikiwa atazingatia vidhibiti vifuatavyo:

1 – Mwanamke huyo ahitajie kazi hiyo au jamii iihitajie kwa njia ya kwamba hakuna mwanaume ambaye anaweza kusimama na kazi hiyo. Kazi hiyo iwe inaendana na maumbile yake.

2 – Hayo yafanyike baada ya kutekeleza kazi zake za nyumbani ambazo kusema kweli ndio kazi zake za msingi.

3 – Kazi hiyo iwe katika mazingira ya wanawake kama mfano wa kuwafunza wanawake, kuwatibu wanawake na kuwauguza wanawake. Awe ni mwenye kujitenga mbali na wanaume.

4 – Hakuna kizuizi, bali ni lazima kwa mwanamke ajifunze mambo yanayohusiana na dini yake. Kama ambavyo hakuna kikwazo vilevile yeye kuwafunza wanawake wenzie mambo yanayohusiana na dini yao ambayo wanayahitajia. Mafunzo hayo yawe katika mazingira ya wanawake. Ni sawa akahudhuria darsa misikitini na kwenginepo, awe ni mwenye kujisitiri na mwenye kujitenga mbali na wanaume kwa mujibu wa vile wanawake walivyokuwa wakifanya hapo mwanzoni mwa Uislamu ambapo wakifundisha, wakijifunza na wakihudhuria misikitini.

[1] 04:27

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 21/10/2019