Twahara inahitaji kitu ambacho mtu atajitwaharisha kwacho kuondosha najisi kwacho na hadathi. Nacho si kingine ni maji. Maji ambayo kwayo ndio twahara inapatikana ni yale maji masafi. Nayo ni yale maji ambayo ni masafi yenyewe kama yenyewe na ni yenye kusafisha kitu kingine. Ni yale maji yaliyobaki katika asili yaliyoumbiwa. Kwa msemo mwingine ni yale mali yaliyobaki katika sifa yaliyoumbiwa. Ni mamoja maji hayo yanateremka kutoka mbinguni, kama mfano wa mvua, theluthi inayoyayuka, maji ya umande, au yoyote yanayopita kwenye maji kama mfano wa maji ya mito, maji ya chemchem, maji ya visima na maji ya bahari. Amesema (Ta´ala):

وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ

“Akakuteremshieni maji kutoka mawinguni ili akutwaharisheni kwayo.”[1]

وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً طَهُورًا

”Tunateremsha kutoka mawinguni maji yaliyo safi.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Nisafishe kutokamana na makosa yangu kwa maji, theluthi na baridi.”[3]

“[Bahari] ni masafi maji yake. Maiti zake zimehalalishwa.”[4]

 Twahara haipatikani kwa vitu vya majimaji visivyokuwa maji kama mfano wa siki, petroli, juisi, limao na vitu mfano wake. Hayo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا

“… na msipate maji, basi kusudieni [fanyeni Tayammum kwa] udongo ulio safi.”[5]

Lau ingelikuwa twahara inapatikana kwa vitu vya majimaji, mbali na maji ya kawaida, basi angepelekwa huko wakati wa kukosekana kwa maji na asingelipelekwa kwenye udongo.

[1] 08:11

[2] 25:48

[3] al-Bukhaariy (744) na Muslim (598).

[4] Abu Daawuud (83), at-Tirmidhiy (69), an-Nasaa´iy (59), Ibn Maajah (3246). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Vilevile imesahihishwa na al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan-in-Nasaa´iy” (58).

[5] 05:06

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 2
  • Imechapishwa: 20/02/2020