03. Lulu kuhusu Ibn Abiy Haatim

3- Ibn Abiy Haatim (kfrk. 327) tabaka 11

adh-Dhahabiy ameandika wasifu wake katika ”Tadhkirat-ul-Huffaadhw” na akasema:

”Imaam, Haafidhwh, mkosoaji na Shaykh-ul-Islaam Abu Muhammad ´Abdur-Rahmaan, mtoto wa Haafidhw mkubwa Abu Haatim Muhammad bin Idriys bin al-Mundhir at-Tamiymiy al-Handhwaliy ar-Raaziy. Imesemekana kwamba amejinasibisha na Handhwal kwa sababu ya barabara ilioko Rayy. Alizaliwa mwaka wa 240. Akasafiri pamoja na baba yake kwa ajili ya kutafuta elimu.

Abu Ya´laa al-Khaliyliy amesema:

”Alisoma kwa baba yake na kwa Abu Zur´ah. Alikuwa ni bahari katika elimu na katika utambuzi juu ya wanaume. Ametunga kuhusu Fiqh na tofauti za Maswahabah na Taabi´uun. Alikuwa ni mwenye kuipa kisogo dunia na anazingatiwa ni katika wenye kuifanya upya dini.

Kitabu chake ”al-Jarh  wat-Ta´diy” kinashuhudia juu ya hifdhi yake ya kipekee. Kitabu chake kuhusu tafsiri ya Qur-aan ni mijeledi. Ana kitabu kikubwa kinachowaraddi Jahmiyyah. Kinathibitisha juu ya uongozi wake.

´Aliy bin Ahmad al-Faradhwiy amesema:

“Simjui yeyote anayemtambua ´Abdur-Rahmaan aliwahi kumuona akitenda dhambi hata siku moja. Imepokelewa namna ambavyo baba yake alikuwa akishangazwa na ´ibaadah za ´Abdur-Rahmaan na akisema: “Ni nani anayefanya ´ibaadah kama ´Abdur-Rahmaan? Sijui kutoka kwake kufanya dhambi yoyote.”

Ibn Abiy Haatim amesema:

“Baba yangu hakuniacha kusoma Hadiyth mpaka nilipohifadhi kwanza Qur-aan kwa al-Fadhwl bin Shaadhaan.”

Abul-Hasan ´Aliy bin Ibraahiym ar-Raaziy amesema:

“Allaah alimvisha (Rahimahu Allaah) uzuri na nuru. Yule mwenye kumtazama hufurahishwa naye. Nilimsikia akisema: “Mimi na baba yangu tulisafiri kwenda hajj ilihali bado sijabaleghe. Tulipofika Dhul-Hulayfah (nje ya al-Madiynah) nikabaleghe. Baba uangu akafurahi kwa sababu hapo ningeweza kuhiji ile hajj ya faradhi.”

´Aliy bin Ahmad al-Khawaarzimiy amesimulia namna Ibn Abiy Haatim alivosema:

“Tulikuwa Misri miezi saba. Katika kipindi chote hicho hatukula kitu cha majimaji. Michana yetu tukiitumia na wanachuoni na nyusiku zetu tukizitumia kuandika na kuulizana yale tuliyojifunza. Siku moja mimi na rafiki yangu tukafika kwa Shaykh. Wakasema kwamba ni mgonjwa. Nikaona samaki mzuri ambapo nikamnunua. Tulipofika nyumbani ilikuwa ni wakati wa darsa la Shaykh mwingine. Tukaenda zetu na tukamwacha samaki akabaki pale kwa muda wa siku tatu na akawa anaenda kukaribia kuoza. Hatukuwa na muda wa kumpika na hivyo tukamla akiwa mkavu. Elimu haifikiwi kwa kustarehe kwa mwili.”

Abul-Hasan amesema:

“Alisafiri pamoja na baba yake na alihiji pamoja na Muhammad bin Hammaad at-Twahraaniy mwaka wa 260. Baada ya hapo akasafiri mwenyewe kwenda Shaam na Misri mwaka wa 262. Mwaka wa 264 akasafiri kwenda Aswbahaan.

Alifariki katika Muharram mwaka wa 327.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tadhkiyr-un-Naabihiyn, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 10/06/2019