03. Kutofautiana kwa washirikina katika waungu wao

Tawhiyd hii ndio msingi katika ulimwengu na shirki imejiingiza ndani yake. Amesema (Ta´ala):

كَانَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً فَبَعَثَ اللَّـهُ النَّبِيِّينَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ فِيمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ

“Watu walikuwa ummah mmoja kisha Allaah akawatuma Mitume hali ya kuwa ni wabashiriaji na waonyaji na akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki ili kihukumu kati ya watu katika ambayo wamekhitilafiana kwayo.”[1]

وَمَا كَانَ النَّاسُ إِلَّا أُمَّةً وَاحِدَةً فَاخْتَلَفُوا ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ فِيمَا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ

”Wala watu hawakuwa isipokuwa ni ummah mmoja kisha wakatofautiana. Na kama si neno lililotangulia kutoka kwa Mola wako,  basi bila shaka ingehukumiwa kati yao katika yale waliyokuwa kwayo wakitofautiana.”[2]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Kati ya Aadam na Nuuh (´alayhimaas-Swalaah was-Salaam) kulikuwa karne kumi. Wote walikuwa juu ya Uislamu.”[3]

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Haya ndio maoni sahihi kuhusiana na Aayah na kumetajwa yenye kuliunga mkono hilo kutoka katika Qur-aan.”[4]

Vilevile Haafidhw Ibn Kathiyr amelisahihisha katika “Tafsiyr” yake.

Mara ya kwanza kuzuka shirki ilikuwa kwa watu wa Nuuh pindi walipochupa mipaka kwa waja wema na wakawa na kiburi juu ya ulinganizi wa Mtume wao:

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

“Wakasema: “Msiwaache waungu wenu na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr.”[5]

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema katika “as-Swahiyh” yake[6] kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Haya ni majina ya waja wema kutoka katika watu wa Nuuh. Wakati walipofariki shaytwaan akawashawishi watu wao watengeneze masanamu katika vikao vyao walivyokuwa wanakaa na wayaite kwa majina ambapo wakafanya hivo. Hayakuabudiwa mpaka walipofariki watu wale na elimu ikasahaulika. Hapo ndipo wakaabudiwa.”

Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Amesema zaidi ya mmoja katika Salaf kwamba: “Walipofariki walikuwa wakikaa kipindi kirefu kwenye makaburi yao kisha wakatengeneza masanamu/picha zao halafu kukapita muda hatimaye wakaabudiwa.”[7]

Kisha akasema:

“Shaytwaan amecheza na washirikina katika kuyaabudu masanamu kila watu kwa kiasi cha akili zao zilivyo.

Kuna kundi amewaita kuyaabudu kwa njia ya kuwaadhimisha wafu ambao walitengeneza masanamu yao kwa picha zao, kama ilivyokuwa kwa watu wa Nuuh. Hii ndio sababu inayokuwa mara nyingi kwa wale washirikina wasiokuwa na elimu. Kuhusu wale wasomi wamejichukulia masanamu kwa aina ya nyota yenye kuathiri, kutokana na vile wanavodai, na wakayafanyia majengo, ngome na pazia. Hayohayo yanaendelea kufanyika tokea hapo kale mpaka hivi sasa. Kimsingi ni kwamba haya ni madhehebu ya washirikina wa as-Swaabi-ah, ambao ni watu wa Ibraahiym (´alayhis-Salaam), ambao alijadiliana nao juu ya ubatili wa shirki na akazivunja hoja zao kwa elimu yake na akawavunja waungu wao kwa kutumia mkono wake. Matokeo yake wakaona wamchome moto.

Kuna kundi lingine ambalo waliufanya mwezi kuwa sanamu na wakadai kuwa ndio ambao unastahiki kuabudiwa na kwamba ndio ambao unaendesha huu ulimwengu wa chini.

Kuna kundi lingine ambalo linaabudu moto, nao si wengine bali ni majusi. Matokeo yake wanaujengea moto mkubwa na wanabaki hapo kwa muda mrefu na kuufanyia ngome madhubuti na pazia. Hawauachi uzime hata mara moja.

Lipo kundi ambalo limeabudu maji huku wakidai kwamba maji ndio msingi wa kila kitu na kwayo ndiko kunapatikana uzalikaji, ukuaji, usafi na usanifu.

Lipo kundi vilevile limeabudu wanyama.

Lipo kundi limeabudu farasi.

Kundi lingine limeabudu ng´ombe.

Kuna kundi lingine limeabudu viumbe waliohai na wafu.

Kuna kundi limeabudu majini.

Lipo kundi pia limeabudu miti.

Vilevile kuna kundi limeabudu Malaika.”[8]

[1] 02:213

[2] 10:19

[3] Tazama ”Tafsiyr-ul-Qur-aan al-´Adhwiym” (01/250) ya Ibn Kathiyr.

[4] Tazama ”Ighaathat-ul-Lahfaan” (02/201).

[5] 71:23

[6] Tazama ”Swahiyh-ul-Bukhaariy” (06/133).

[7] Tazama ”Ighaathat-ul-Lahfaan” (02/202).

[8] Tazama ”Ighaathat-ul-Lahfaan” (02/218-233).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 05-08
  • Imechapishwa: 04/02/2019