03. Kujitenga na mambo ya ubishi na kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“… kuepuka mivutano na kuepuka kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´… “

MAELEZO

Bi maana miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah waliyoshikamana nayo barabara na hawakugeuza wala kubadilisha yale waliyohifadhi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); Qur-aan na Sunnah. Hakuna nafasi yoyote ya mijadala na mizozo, kama wafanyavyo Ahl-ul-Bid´ah wapotevusiku zote na kila mahali ambapo wao wanachotaka ni fitina. Makusudio ya mivutano na mijadala iliyokatazwa ni mivutano katika dini ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) pasi na malengo ya sawa wala makusudio mazuri. Vinginevyo mijadala iliotokea kati ya Mitume na nyumati zao na Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah. Mivutano ya Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah inahusiana na kuzibainisha hali zao, kuwasimamishia hoja, kuraddi Bid´ah na upotofu wao na kutahadharisha nao. Wanatosheka na hilo. Hawafanyi vikao vingi pamoja na Ahl-ul-Ahwaa´. Wanawanasihi kwa kuwanainishia Sunnah na kuwaamrisha kushikamana nayo, kuzibainisha Bid´ah zao na kutahadharisha nao. Wanawaraddi sawa ikiwa ni kwa njia ya maneno au uandishi. Hivo ndivo walivyofanya wanachuoni waliotangulia, isiwe zaidi wala chini ya hapo.

Kuhusu Ahl-us-Sunnah kujadiliana na Ahl-ul-Bid´ah, ni jambo lina lengo la Kishari´ah. Mtu anakuwa anamtakia kheri yule ambaye amepatwa na maradhi ya utata ili haki iweze kumbainikia. Mjadala unaweza kuwa unazungumzia ´Aqiydah au ´ibaadah. Mjadala unaweza kufanywa kwa ajili ya kuinsuru Sunnah ambayo ndio yenye haki zaidi ya kufuatwa.

Ama mijadala mingi kwa ajili ya kushinda au kwa ajili ya kusapoti mrengo fulani unaokwenda kinyume na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah au Bid´ah, Ahl-us-Sunnah wanajiepusha na vikao vya watu hawa ambao lengo lao sio haki na kuitendea kazi. Ajenga yao ni kutaka kuwapaka watu mchanga wa machoni na kuwapotosha wajinga ili mwishowe waweze kujiunga nao, Ahl-ul-Bid´ah na wapotofu.

Mtu ambaye ni Sunniy akitoa nasaha na akaeneza elimu na Sunnah ambapo ujumbe wake ukakubaliwa, basi lengo limefikiwa. Ama yule mwenye kuanza kuleta ubishi na akajibabaisha mwenyewe na akataka kuwababaisha wengine, basi mtu huyu Ahl-us-Sunnah wanaachana naye. Kadhalika wanaachana na upotoshaji na ubabaishaji wake na wanawatahadharisha watu kutokamana naye.

Kwa hiyo kuna mijadala aina mbili:

1- Ubishi ulioamrishwa na wenye kusifiwa. Katika hali hii yule mwenye kufanya mjadala anapewa thawabu. Mjadala huu unahusiana na kuibainisha na kuiweka wazi haki na kuiraddi batili kwa kutumia dalili za Qur-aan na Sunnah. Ubishi huu ni ule ambao Allaah ameuidhinisha pale aliposema:

وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“… na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[1]

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Msijadiliane na Ahl-ul-Kitaab isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi.”[2]

2- Ubishi wenye kusemwa vibaya, hivi ndivo wafanyavyo Ahl-ul-Bid´ah na wapotofu na makafiri hapo kabla yao. Ubishi wao unahusiana na kuisaga haki. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

مَا يُجَادِلُ فِي آيَاتِ اللَّـهِ إِلَّا الَّذِينَ كَفَرُوا

“Habishani kuhusu Aayah za Allaah isipokuwa wale waliokufuru.”[3]

Ubishi wa Ahl-ul-Bid´ah umefanana na ubishi wa makafiri. Malengo yao ni kuisambaratisha Sunnah ili Bid´ah na upotevu viweze kuchukua nafasi yake, jambo ambalo linaenea shari yenye kuenea.

Huu ndio ule ubishi wenye kusemwa vibaya, ni mamoja uwe umetoka kwa makafiri au umetoka kwa Ahl-ul-Bid´ah. Kila tendo la jinai lina malipo yake mbele ya Allaah. Mtu wa Bid´ah ima ainusuru na kuisapoti Bid´ah ya kikafiri ambayo inamtoa mwenye nayo nje ya Uislamu au akafanya propaganda za kulingania katika Bid´ah ambayo ni khatari ambayo ni zaidi ya dhambi kubwa japokuwa si yenye kumtoa mwenye nato nje ya Uislamu.

Kupitia upekuzi wa kisomi wanachuoni wamethibitisha kwamba madhambi mazito yanaweza kupangiliwa ifuatavyo:

1- Shirki kubwa na kufuru kubwa. Hizi ndio dhambi kubwa kabisa.

2- Shirki ndogo na kufuru ndogo.

3- Bid´ah kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameziita kuwa ni upotevu.

4- Madhambi makubwa na yenye kuangamiza.

5- Madhambi madogo. Yanakuwa makubwa kwa kule mtu kuyaendeleza.

Mpaka hapa tunapata kujua khatari ya Bid´ah na khatari ya wazushi. Wanajiweka khatarini wao wenyewe na Ummah. Kwa ajili hiyo mtu hatakiwi kufanya mchezo wala kuchukulia wepesi suala la Bid´ah hata siku moja. Wala hatakiwi kufanya hivo kwa madhambi, ni mamoja yale makubwa au madogo. Kwa sababu madhambi yanamkasirisha Mola na yanasababisha yule mtenda madhambi kuadhibiwa duniani na Aakhirah.

[1] 16:125

[2] 29:46

[3] 40:04

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 30/09/2019