Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tunaonelea kuwa Sunnah imejengwa juu ya kushikamana na yale waliyokuwemo Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwaiga, kujiepusha na Bid´ah… “

MAELEZO

Pindi tutapojua kuwa ni wajibu kwa waislamu wote kujiepusha na Bid´ah – na kwa walinganizi ni wajibu zaidi kujiepusha nazo – tutatambua ya kwamba ni jambo muhimu linalomuhusu muislamu. Moja katika Bid´ah za khatari hii leo ni propaganda zinazofanywa na ukundi na vyama. Allaah amezikemea katika Aayah nyingi na ameamrisha Ummah uwe kitu kimoja kwa kuwa wana dini moja, wanamwabudu Mola mmoja na wanamfuata Mtume mmoja. Kwa ajili hiyo ni wajibu kwao wote kujiepusha na Bid´ah hizi zinazoufarikisha Ummah na kuutawanyisha katika makundi. Allaah (Ta´ala) amesema:

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ كَبُرَ عَلَى الْمُشْرِكِينَ مَا تَدْعُوهُمْ إِلَيْهِ ۚ اللَّـهُ يَجْتَبِي إِلَيْهِ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَن يُنِيبُ

“Amekuwekeeni katika dini yale aliyomuusia kwayo Nuuh na ambayo tumekuteremshia Wahy wewe na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni dini na wala msifarikiane humo. Yamekuwa magumu kwa washirikina yale unayowalingania. Allaah anamteua Kwake amtakaye na anamuongoza Kwake yule anayejirejea.”[1]

Aayah hii inathibitisha ya kwamba msingi wa dini na Shari´ah ya Allaah kwa wale Mitume bora imejengwa juu ya misingi miwili:

1- Kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall).

2- Ummah uwe kitu kimoja:

أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ

“Simamisheni dini na wala msifarikiane humo.”

Allaah amesema kuwa haya ndio waliyofunuliwa Mitume wote na khaswa wale Mitume watano wakubwa; Muhammad na kabla yake Nuuh, Ibraahiym, Muusa na ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Ikiwa nyujumbe zote hizi zilikuwa ni zenye kuafikiana juu ya misingi hii miwili, ina maana ya kwamba ni katika uwajibu ulio mkubwa kabisa. Kwa ajili hii ndio maana Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja; Nami ni Mola wenu, hivyo basi niabuduni.”[2]

وَإِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja Nami ni Mola wenu, hivyo basi nicheni.”[3]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amewakemea wale wenye kufarikiana na kusema:

فَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ زُبُرًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

“Wakakatakata makundi na kufarikiana kuhusu dini yao, kila kundi kwa waliyomo linafurahia.”[4]

Aayah hizi zinakemea mfumo wa uchama na ukundi na inaamrisha kuwa kitu kimoja na kutofarikiana katika dini. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

“Hakika wale waliofarakisha dini yao na wakawa makundi makundi, huna lolote kuhusiana nao. Hakika amri yao iko kwa Allaah, kisha atawajulisha kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[5]

Aayah hii inawakemea vikali Hizbiyyuun wanaolingania katika mfarakano, jambo ambalo linadhihiri zaidi pale Allaah alipomtakasa Mtume Wake kutokamana na wao na kusema:

لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ

“… huna lolote kuhusiana nao.”

Kutokana na haya inatupasa kutambua kuwa mfumo wa makundi haya yote ni maradhi na upotevu na kwamba uokozi unapatikana katika kufuata Kitabu cha Allaah, njia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam), makhaliyfah wake waongofu na matendo ya Maswahabah waliobaki.

[1] 42:13

[2] 21:92

[3] 23:52

[4] 23:53

[5] 06:159

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 68-69
  • Imechapishwa: 27/01/2017