03. Kosa la tatu katika ´Aqiydah: Kuwaomba viumbe yale wasiyoyaweza

3- Kuwaomba wafu, viumbe walioko mbali, majini, masanamu, miti na mawe, kuwataka msaada, kuwaomba wawaponye wagonjwa na nusura dhidi ya maadui. Hii ndio dini ya washirikina wa kale katika makafiri wa ki-Quraysh na wengineo. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[1]

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Mwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini. Zindukeni! Ni ya Allaah pekee dini iliyotakasika; na wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah ukaribu. Hakika Allaah atahukumu kati yao katika yale waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah hamwongoi aliye mwongo, kafiri mkubwa.”[2]

Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hii. Zote zinafahamisha kwamba washirikina wa kale walikuwa wakitambua kuwa Allaah ndiye mwenye kuumba, mwenye kuruzuku, mwenye kunufaisha na kudhuru. Walikuwa wakiwaomba waungu wao ili wawaombee kwa Allaah na wawakurubishe ukuruba. Allaah akawakafirisha kwa jambo hilo na akawahukumu ukafiri na shirki yao na pia akamwamrisha Mtume Wake kuwapiga vita mpaka wamwabudu Allaah pekee. Amesema (Subhaanah):

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ

“Na piganeni nao mpaka kusiweko shirki na dini yote iwe kwa ajili ya Allaah.”[3]

Wanachuoni wameandika juu ya hilo vitabu vingi na wakaweka wazi uhakika wa Uislamu ambao Allaah amemtumiliza Mtume Wake na akateremsha Vitabu Vyake kwa ajili yake. Pia ndani yake wamebainisha dini ya watu wa kipindi cha kikafiri, imani yao na matendo yao yanayopingana na Shari´ah ya Allaah. Kama mfano wa ´Abdullaah bin Imaam Ahmad, imamu mkubwa Muhammad bin Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd”, Muhammad bin Wadhdhwaah na maimamu wengine. Miongoni mwa yaliyoandikwa juu ya hilo ni yale aliyoandika Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika vitabu vyake vingi. Miongoni mwa vifupi ni kitabu chake ”al-Qaa´idah al-Jaliyyah fiyt-Tawassul al-Wasiylah”. Katika hayo ni yale aliyoandika Shaykh ´Abdur-Rahmaan bin Hasan bin Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahum Allaah) katika kitabu chake ”Fath-ul-Majiyd Sharh Kitaab-it-Tawhiyd”.

[1] 10:18

[2] 39:02-03

[3] 08:39

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Akhtwaau fiyl-´Aqiydah, uk. 2-3
  • Imechapishwa: 20/06/2020