03- Kabla ya Ihraam


1- Imependekezwa kwa yule anayetaka kuhiji, au kufanya ´Umrah iliopekee, kuoga kwa ajili ya Ihraam. Inahusiana vilevile na mwanamke mwenye hedhi au mwanamke mwenye damu ya uzazi.

2- Baada ya hapo wanaume watavaa mavazi wanayoyataka ambayo hayakushonwa kwa kiasi cha viungo. Hizo ndizo zile nguo ambazo Fuqahaa´ wanaziita “zisizoshonwa”. Kwa hivyo avae Izaar, Ridaa´ na viatu. Viatu ni kila kile kinachovaliwa miguuni kilicho juu ya kongo mbili za miguu kwa ajili ya kuilinda miguu.

3- Haifai kwa wanaume kuvaa kofia, kilemba na mfano wa hivyo katika vile vinavyofunika kichwa moja kwa moja.

Kuhusu mwanamke hatavua chochote katika mavazi yake yanayokubalika katika Shari´ah. Hata hivyo asivae Niqaab[1], Burqa´, Lithaam, kitambaa wala vifuniko vya mikononi (gloves). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muhrim asivae kanzu, kilemba, burnus, suruwali, wala nguo ambayo imepakwa na Was (mti wa umanjano) au zafarani wala soksi isipokuwa ikiwa kama hakupata viatu. Katika hali hiyo avae soksi[2].”

Amesema vilevile:

“Mwanamke ambaye ni Muhrim hatovaa Niqaab wala vifuniko vya mikono.”

Hata hivyo inafaa kwa mwanamke kujifunika uso wake kwa kitu chochote kama mtandio au jilbab atayoiteremsha kichwani mwake na kufunika uso wake. Haya hata kama itagusa uso kutokana na maoni yaliyo sahihi. Hata hivyo asiifunge juu ya uso, kama alivyosema Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah).

4- Inafaa kwake yeye kuvaa Ihraam yake kabla ya Miyqaat, ijapokuwa nyumbani kwake. Hayo yalifanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Katika hili kuna wepesi kwa wale wanaosafiri kwa ndege na ikawa haiwezekani kwao kuvaa Ihraam wakati wa Miyqaat. Hata hivyo wasinue Ihraam isipokuwa kabla ya kufika Miyqaat kwa kidogo ili isije kuwapita Miyqaat ilihali sio wenye kuhirimia.

5- Inafaa kwake yeye kupaka mafuta na kujitia manukato katika kiwiliwili chake kwa aina yoyote ile ya manukato yaliyo na harufu na yakawa hayana rangi. Haya hayawahusu wanawake. Manukato yao ni yale yaliyo na rangi na yakawa hayana harufu. Haya yote yanatakiwa kufanyika kabla ya kunuia Ihraam wakati wa Miyqaat kwa sababu ni haramu kufanya hivo baada yake.

[1] Ni mtandio unaogusa pua na unaweza kuwa kwa aina mbalimbali: 1) Mwanamke akipandisha Niqaab yake mpaka kwenye macho yake, hiyo inaitwa Waswasah au Burqaa´. 2) Akiishusha mpaka chini ya macho kidogo, inaitwa Niqaab. 3) Ikiwa kwenye ncha ya mdomo, inaitwa Lithaam. Niqaab imepata jina hilo kwa sababu inafunika rangi ya mwili. Tazama “Linaas-ul-´Arab” (02/265-266).

[2] Shaykh-ul-Islaam ibn Taymiyyah amesema katika “al-Mansik” yake, uk. 365:

“Wala sio wajibu kwake kuzikata chini ya vifundo viwili vya miguu. Mara ya kwanza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha mtu azikate. Baada ya hapo akaruhusu hilo katika ´Arafah mtu avae suruwali ikiwa hakupata Izaar yoyote na soksi kwa yule ambaye hakupata viatu. Haya ndio maoni sahihi zaidi katika rai mbili za wanachuoni.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 19/08/2017