03. Imani inazidi kwa matendo mema na inashuka kwa maasi

Aayah nyingine inayothibitisha kuongezeka kwa imani ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ

“Yeye Ndiye ambaye kateremsha utulivu katika nyoyo za waumini ili awazidishie imani pamoja na imani zao.” 48:04

Hii ni dalili ya wazi juu ya kuongezeka kwa imani.

Imani inazidi kwa matendo ya moyo na inazidi kwa matendo ya viungo vya mwili. Pindi unapomwogopa Allaah imani yako inazidi na hivyo unaanza kuswali, kufunga, kutoa zakaah, kuhiji, kuwatendea wema wazazi wawili, kuamrisha mema, kukataza maovu na kuutamania Uislamu na waislamu kheri. Yote haya yanaifanya imani kuzidi na inaweza kupanda mpaka ikawa kama mlima. Aayah inathibitisha kuwa imani inaongezeka. Hata hivyo kuna Aayah nyingi zinazothibitisha hilo.

Vilevile kuna Hadiyth zinazofahamisha pia kuwa imani inashuka kukiwemo Hadiyth zilizopokelewa kwa mapokezi mengi kuhusu uombezi. Kwa mfano:

“Mtoeni Motoni yule ambaye moyoni mwake mna imani sawa na uzito wa dinari, kisha yule ambaye yuko na imani sawa na uzito wa nusu ya dinari, kisha yule ambaye yuko na imani sawa na uzito wa shayiri, halafu yule ambaye yuko na imani sawa na uzito wa mbegu halafu yule ambaye yuko na imani chini, chini na chini kabisa kuliko uzito wa mbegu.” al-Bukhaariy (7439) na Muslim (183).

Ni kipi chenye kufanya ikapungua? Ni maasi kwa sababu yake wataingia Motoni. Hata hivyo Allaah atawatoa Motoni kwa sababu ya upwekeshaji wao:

“… halafu yule ambaye yuko na imani sawa na uzito wa mbegu halafu yule ambaye yuko na imani chini, chini na chini kabisa kuliko uzito wa mbegu.”

Allaah akitaka kuwaadhibu wale waliotumbukia katika zinaa, kuiba, kupora, kueneza ufisadi katika ardhi, kudhulumu na kula ribaa, atafanya hivo. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah. Hawakufurishi kwa maasi na wala hawawahukumu watenda madhambi kudumu Motoni milele kama wanavyofanya Khawaarij ambao wanatupilia mbali uombezi wa waombezi.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 08-11
  • Imechapishwa: 09/10/2016