Ni kweli kwamba mapote, makundi, madhehebu na maoni ni mengi. Hii ni dini ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka – hivyo basi, ifuateni – na wala msifuate vijia vya vichochoro vikakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni kwayo mpate kuogopa.”[1]

Njia ya Allaah ni ile ambayo Allaah alimtuma kwayo Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ikafuatwa na Maswahabah zake watukufu, karne bora na waliokuja nyuma ambao walifuata athari zao mpaka Qiyaamah kisimame. Hiyo ndio njia ya Allaah. Ama yale yanayokwenda kinyume na njia hii basi hivyo ndivo vijia vya vichochoro.

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwahi siku moja kupiga msitari uliyonyooka. Pembezoni na msitari huo akachora njia nyingi. Akasema (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) juu ya ile njia iliyonyooka: “Hii ndio njia ya Allaah.” Halafu akasema kuhusu zile njia mbalimbali za kupinda zilizokuwa pembezoni: “Njia zengine hizi ni vichochoro na katika kila kichochoro kuna shaytwaan anayelingania kwacho.”[2]

Huu ni ubainifu wa wazi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Aayah tukufu ifuatayo:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ

“Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka – hivyo basi, ifuateni.”

Kwa hivyo watu walio na ´Aqiydah sahihi na watu waliookoka na upotevu, Moto na kutokamana na matamanio ni kundi moja pekee. Nao si wengine ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Tunamuomba Allaah atujaalie sisi na nyinyi kuwa katika wao, atukusanye nao na atujaalie kufuata uongofu wao mpaka siku tutakutana Naye.

[1] 06:153

[2] Ahmad (01/435) na ad-Daarimiy (202).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 04
  • Imechapishwa: 24/05/2022