Ee waislamu! Hakika umekujieni mwezi mtukufu  na uliobarikiwa, nao si mwengine ni wa kufunga Ramadhaan. Ni mwezi ambao watu wanasimama usiku na kuswali. Katika mwezi huo wako ambao wanaachiwa huru na Moto na wengine wanasamehewa madhambi. Katika mwezi huo watu hutoa swadaqah na kufanya matendo mema. Katika mwezi huo milango ya Pepo inafunguliwa na matendo mema yanalipwa zaidi na zaidi. Katika mwezi huo madhambi yanapungua. Du´aa zinaitikiwa. Watu wanapandishwa daraja. Madhambi yanasamehewa. Katika mwezi huo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) huwatunuku waja Wake neema mbalimbali na mawalii Wake hupata zawadi tele. Allaah amefanya kufunga mwezi huo ni moja katika nguzo za Uislamu. Mteuliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliufunga na akawaamrisha watu wafunge. Ameeleza kwamba yule ambaye ataufunga na kusimama nyusiku zake hali ya kuwa na imani na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah, basi Allaah atamsamehe madhambi yake yaliyotangulia. Katika mwezi huu kuna usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu moja. Atayenyimwa kheri zake kwa kweli huyo amenyima.

Ramadhaan ina fadhila na sifa za kipekee nyingi. Miongoni mwazo ni zile alizopokea Imaam Ahmad kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ummah wangu umepewa sifa tano katika Ramadhaan ambazo hakuna Ummah walipewa kabla yake; harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski, Malaika wanawaombea msamaha mpaka wakate swawm, majini waovu wanafungwa minyororo ili wasifanye yale wanayoweza kufanya, Allaah huipamba Pepo Yake kila siku na kusema: “Karibu waja Wangu wema watasalimika kutokamana na maudhi na matatizo na kuja Kwako” na wanasamehewa mwishoni mwa usiku.” Kukasemwa: “Usiku wa Qadar?” Akasema: “Hapana. Mtendaji hupata ujira wake pale anapomaliza kitendo chake.”[1]

“Inapofika siku ya kwanza ya Ramadhaan mashaytwaan hufungwa minyororo na majini waovu hufungwa. Milango ya Moto hufungwa na hakuna unaofunguliwa na milango ya Pepo hufunguliwa na hakuna unaofungwa. Hunadi Mwenye kunadi: “Wewe unayetafuta kheri! Njoo! Wewe unayetafuta shari! Koma!” Kila usiku Allaah huwaacha huru watu fulani kutokamana na  Moto.”[2]

“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, mwezi wa baraka. Allaah huwafunikeni, huteremsha rehema, hufuta madhambi na huitikia du´aa ndani yake. Allaah hutazama namna mnavyoshindana ndani yake na hujifakhari kwenu mbele ya Malaika Zake. Kwa hivyo muonyesheni Allaah yale mazuri yenu. Hakika mla khasara ni yule mwenye kunyimwa rehema za Allaah.”[3]

“Atayefunga Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Atayesimama usiku wa Qadar kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[4]

“Kila tendo jema la mwanaadamu linalipwa mara kumi mpaka mara mia saba. Allaah akasema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu na mimi Ndiye nitayeilipa. Ameacha matamanio Yake na chakula Chake na kinywaji Chake kwa ajili Yangu.” Mfungaji ana furaha mbili; furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm yake na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola Wake. Harufu ya mfungaji inapendwa zaidi na Allaah kuliko hafuru ya miski.”[5]

Hadiyth zinazozungumzia juu ya swawm ya Ramadhaan, kuswali nyusiku zake na jinsia ya swawm ni nyingi. Kwa hiyo muumini anatakiwa aitumie fursa hii. Kukutana na mwezi wa Ramadhaan ni neema kutoka kwa Allaah. Akimbilie katika matendo mema na ajiepushe na madhambi na ajitahidi kutekeleza yale Allaah aliyomfaradhishia juu yake.

Tahadharini – Allaah akurehemuni – na yale yote yanayoidhuru swawm, kupunguza thawabu zake na kumkasirisha Mola (´Azza wa Jall) kama mfano wa ribaa, zinaa, kuiba, kuua kulikoharamishwa, kula mali ya mayatima na aina nyenginezo za dhuluma zinazohusiana na nafsi, mali na heshima, ghushi, khiyana, kuwaasi wazazi wawili, kukata udugu, chuki, kukatana kimakosa, kunywa pombe, madawa ya kulevya kama Qaat na sigara, kusengenya, uvumi, uongo, ushahidi wa uongo, madai batili, viapo vya uongo, kupunguza au kunyoa ndevu, kurefusha masharubu, kuwa na kiburi, nguo ya mwanaume yenye kuvuka kongo mbili za miguu, muziki, wanawake kutoka na nguo za mapambo, kutojisitiri kutokamana na wanaume na kujifananisha na wanawake wa makafiri inapokuja katika mavazi na kuvaa mavazi mafupi na mengine yote ambayo Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamekataza.

Madhambi yote haya yaliyotajwa ni haramu pasi na kujali zama na pahali, lakini katika Ramadhaan ni khatari na makubwa zaidi kutokamana na fadhila na heshima yake. Kwa hiyo mcheni Allaah, enyi waislamu, na jiepusheni na yale Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamekukatazeni. Hakikisheni mmeendelea kumtii katika Ramadhaan na miezi mingine. Peaneni nasaha na saidianeni juu ya hilo. Amrisheni mema na katazeni maovu ili muweze kupata Pepo, furaha, utukufu na kufuzu duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atukinge sisi, nyinyi na waislamu wengine wote kutokamana na yale yenye kusababisha hasira Zake na atukubalie swawm na visimamo vyetu sote, azitengeneze hali za watawala wa waislamu na ainusuru dini Yake kupitia wao  na awakoseshe nusura maadui Wake kupitia wao na awafanye wote kuielewa dini na kuwa na msimamo juu yake na kuhukumu kwayo katika mambo yote. Hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza. Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na wale wote wenye kupita juu ya uongofu wake mpaka siku ya Qiyaamah. Tunamuomba Allaah atulinde sisi na nyinyi kutokamana na uovu wa nafsi na matendo yetu. Tunamuomba Allaah awaongoze watawala wetu sisi na watawala wengine wote wa waislamu kwa yale anayoyapenda na kuyaridhia na ainusuru haki kupitia wao na aiangushe batili kupitia wao. Tunamuomba Awakinge wote kutokamana na fitina zenye kupotosha. Hakika Yeye ni muweza juu ya hilo. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah wake.

[1] al-Bayhaqiy katika ”Fadhwaa’il-ul-Awqaat” (1/144) na al-Haytamiy katika ”al-Majma´” (4778). Dhaifu sana kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dha´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (586).

[2] at-Tirmidhiy (682), Ibn Maajah (1642) na al-Haakim (1532). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy i ”Swahiyh-ul-Jaami´” (759).

[3] at-Twabaraaniy katika ”Musnad-ush-Shaamiyyiyn” (2238). Imezuliwa kwa mujibu wa al-Albaaniy  katika ”Dhwa´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (592).

[4] al-Bukhaariy (1901) na (2014) bila ya ”Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan…” na vilevile Muslim (670). Hadiyth imepokelewa kikamilifu na at-Tirmidhiy (683) na Ahmad (10159).

[5] al-Bukhaariy (7492) na Muslim (1151).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mufiyd fiy Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 5-7
  • Imechapishwa: 02/04/2022