03. Dalili za uwajibu wa kufuata Sunnah

Msingi wa pili miongoni mwa misingi mitatu ambayo kuna maafikiano juu yake ni yale yaliyosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanachuoni na watu wa imani waliokuja baada yao. Wanaamini msingi huu mkubwa, wanautumia kama dalili na kuufunza nao Ummah. Wameandika juu ya hilo vitabu vingi na kuliweka wazi katika vitabu vya Fiqh na vya istilahi. Dalili juu ya hilo hazidhibitikiwi kutokana na wingi wake. Miongoni mwa dalili hizo ni yale yaliyokuja katika Qur-aan tukufu juu ya maamrisho ya kumfuata na kumtii. Hilo linawahusu wale waliokuwa katika kipindi chake na wataokuja baada yao. Yeye ni Mtume wa Allaah kwa walimwengu wote. Sababu nyingine vilevile ni kuwa wameamrishwa kumfuata na kumtii mpaka pale Qiyaamah kitaposimama. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwenye kuifasiri Qur-aan na kuyaweka wazi yale yaliyo kwa jumla. Anafanya hivo kwa maneno, matendo na yale aliyoyakubali.

Pasi na Sunnah waislamu wasingelitambua idadi ya Rakaa´ za swalah, namna yake na yale ya wajibu ndani yake. Vilevile wasingelijua upambanuzi wa hukumu za swawm, zakaah, hajj, Jihaad, kuamrisha mema na kukataza maovu. Aidha pia wasingelitambua upambanuzi wa hukumu za mambo ya biashara, yaliyo ya haramu na mipaka na adhabu za Kishari´ah ambazo Allaah kaziwajibisha. Baadhi ya Aayah zilizothibiti ni maneno Yake (Ta´ala) katika Suurah “Aal ´Imraan”:

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

”Mtiini Allaah na Mtume mpate kurehemewa.” (03:132)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖفَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wale wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.” (04:59)

Amesema (Ta´ala) vilevile katika Suurah “an-Nisaa´”:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا

“Atakayemtii Mtume basi hakika amemtii Allaah na atakayekengeuka, hatukukutuma kuwa mlinzi juu yao.” (04:80)

Itawezekanaje kumtii na kurudisha yale ambayo watu wamezozana kwayo katika Qur-aan na Sunnah ikiwa Sunnah hazitumiwi kama hoja au ikiwa zote si Swahiyh? Kwa mujibu wa maneno haya itakuwa Allaah amewaelekeza waja katika kitu ambacho hakipatikani. Hii ni batili kubwa na ni aina kubwa ya kumkufuru Allaah na kumjengea dhana mbaya. Amesema (´Azza wa Jall) katika Suurah “an-Nahl”:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na huenda wakapata kuzingatia.” (16:44)

وَمَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ إِلَّا لِتُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي اخْتَلَفُوا فِيهِ ۙ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

”Hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa ili uwabainishie yale waliyokhitilafiana kwayo na pia iwe ni mwongozo na Rahmah kwa watu wanaoamini.” (16:64)

Ni vipi Allaah atampa Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kazi ya kubainisha kile wanachoteremshiwa ikiwa Sunnah haina maana yoyote? Amesema tena katika Suurah “an-Nuur”:

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

”Sema: “Mtiini Allaah na mtiini Mtume.” Mkikengeuka, basi hakika ni juu yake yale aliyobebeshwa na ni juu yenu yale mliyobebeshwa. Na hakika mkimtii mtaongoka – na hapana linalomlazimu Mtume isipokuwa kufikisha kuliko wazi.” (24:54)

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

”Simamisheni swalah na toeni zakaah na mtiini Mtume ili mpate kurehemewa.” (24:56)

Amesema (Ta´ala) katika Suurah “al-A´raaf”:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖفَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote; [Allaah] pekee Aliye na ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye – Anahuisha na kufisha. Basi mwaminini Allaah na Mtume wake; Nabii asiyejua kusoma wala kuandika ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake na mfuateni ili mpate kuongoka.” (07:158)

Katika Aayah hizi kuna dalili za wazi zinazoonyesha kwamba uongofu na rehema vinapatikana kwa kumfuata (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vipi hayo yatawezekana bila ya kutendea kazi Sunnah zake au kusema kuwa si sahihi au hazitegemewi? Amesema (´Azza wa Jall) katika Suurah “an-Nuur”:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije ikawapata fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo.” (24:63)

Amesema katika Suurah “al-Hashr”:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Kile alichokupeni Mtume kichukueni na kile alichokukatazeni kiacheni.” (59:07)

Kuna Aayah nyingi zilizo na maana kama hii ambazo zote zinathibitisha juu ya uwajibu wa kumtii (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kufuata yale aliyokuja nayo, kama zilivyotangulia dalili juu ya uwajibu wa kuifuata Qur-aan, kushikamana nayo na kutii maamrisho na makatazo yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ujuwb-ul-´Amal bis-Sunnah
  • Imechapishwa: 23/10/2016