Kujionyesha kumegawanyika aina mbili:

1- Kujionyesha ambako ni shirki kubwa. Hivo inakuwa pale ambapo makusudio ya mtu kwa matendo yake yote ni kuwaonyesha watu na sio kwa ajili ya Allaah kabisa. Lengo lake anataka kuishi na waislamu, ilindwe damu yake na uhifadhike mali yake. Huku ndio kujionyesha kwa wanafiki na ni shirki kubwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا

“Hakika wanafiki wanafikiri wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu.”[1]

Aina kama hii haitoki kwa muislamu.

2- Kujionyesha kunakoweza kutoka kwa muumini na kukampata baadhi ya matendo yake. Hali inakuwa hivo pale ambapo kitendo kinafanywa kwa kumlenga Allaah na kumlenga mwengine asiyekuwa Allaah. Hii ndio shirki ndogo. Kujionyesha aina hii kumegawanyika aina tatu:

1- Kitendo kikafanywa kwa kujionyesha kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho wake. Kitendo hichi ni chenye kurudishwa na hakikubaliwi na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mwenye kuswali kwa ajili ya Allaah na wakati huohuo anataka asifiwe na kujionyesha kukaendelea mpaka mwishoni mwa swalah, swalah yake haikubaliwi. Dalili ya hilo ni Hadiyth itayokuja huko mbele.

2- Msingi wa kitendo kimefanywa kwa ajili ya Allaah kisha baadaye kikaingiliwa na kujionyesha. Mtu kama huyu papo kwa hapo akitubia kwa Allaah, akapambana na akaendelea kufanya kitendo chake hali ya kumtakasia nia Allaah, kuna maafikiano kwamba hakutomdhuru.

3- Kujionyesha kukazuka katikati ya kitendo na kukaendelea mpaka mwisho. Wanachuoni wametofautiana katika hili. Wako waliosema kwamba kitendo kinabatilika, kama ile hali ya kwanza. Wengine wakasema kwamba atalipwa thawabu kwa kiasi cha alivyomtakasia Allaah nia. Ibn Rajab ametaja upambanuzi kwa kina katika “Jaaamiy´-ul-´Uluum wal-Hikam”.

[1] 04:142

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 440
  • Imechapishwa: 26/08/2019