02. Uwajibu wa mja katika dini yake

Lililo la wajibu juu ya mja katika dini yake ni kufuata yale yaliyosemwa na Allaah (Ta´ala), Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), makhaliyfah waongofu kati ya Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema.

Allaah amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa dalili na mwongozo. Akawawajibishia watu wote wamuamini yeye na wamfuate kwa dhahiri na kwa siri. Amesema (Ta´ala):

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعاً الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ فَآمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Sema: “Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote wa [Yule] ambaye pekee anao ufalme wa mbingu na ardhi! Hapana mungu wa haki ila Yeye – Anahuisha na anafisha. Basi mwaminini Allaah na Mtume Wake, ambaye hajui kuandika wala kusoma, ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake na mfuateni ili mpate kuongoka.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu. Tahadharini na mambo ya kuzusha. Hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[2]

Makhaliyfah waongofu ni wale waliomrithi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika elimu yenye manufaaa na matendo mema. Ambao wana haki zaidi ya sifa hii ni Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Kwani hakika Allaah amewateua ili wasuhubiane na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wasimamishe dini Yake. Allaah (Ta´ala) – ambaye ni Mjuzi wa yote na Mwenye hekima – asingelichagua usuhubiano na Mtume Wake lau usingelikuwa na imani kamilifu, akili yenye nguvu, kitendo bora, maazimio yaliokomaa na njia iliyonyooka kabisa. Kwa hivyo wakawa ndio wenye haki zaidi ya kufuatwa baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada yao wanakuja maimamu wa dini ambao wamejulikana kwa uongofu na wema.

[1] 07:158

[2] at-Tirmidhiy (2676), Abu Daawuud (4607) na Ibn Maajah (42). at-Tirmidhiy amesema:

“Hasan (nzuri) Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 06-08
  • Imechapishwa: 06/01/2020