02. Uwajibu wa kufuata njia ya waumini

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tunaonelea kuwa Sunnah imejengwa juu ya kushikamana na yale waliyokuwemo Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwaiga… “

MAELEZO

Maana yake ni kwamba tunatakiwa kuwafuata Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuitakidi kuwa wao ndio wabora wa Ummah wanaopendwa zaidi na Allaah na ambao wako karibu Naye zaidi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Atakayempinga Mtume baada ya kumbainikia uongofu na akafuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamwacha aelekee huko alikoelekea na [baadaye] Tutamwingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kuishia.”[1]

Maneno Yake:

وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ

“… na akafuata njia isiyokuwa ya waumini… “

anawakusudia Maswahabah. Maswahabah ndio watu walio na imani yenye nguvu kabisa na wenye nafasi za juu kabisa kwa Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mkononi mwake lau mmoja wenu atajitolea dhahabu mfano wa Uhud haitofikia mikono miwili iliyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”[2]

Waumini wanaokusudiwa katika Aayah ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anayechagua kufuata njia au mwengine asiyekuwa wao basi amepotea na kupotea. Inatosha kwa Allaah kumwacha, aelekee huko alikoelekea na kumvugumiza Motoni ambapo ni mahali pabaya kabisa.

Haya yanazidi kutilia mkazo ya kwamba ni wajibu kwa kila mwanafunzi kufuata njia ya wuamini, ambao ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na siku zote anatakiwa kufikiria matishio haya. Kuna Ikhwaaniy mmoja aliyesema:

al-Ikhwaan wana mnara

Yote yaliyomo ndani yake ni mazuri

Usiulize ni nani aliyeujenga

Ulijenga Hasan

Hebu tuangalie kama yale aliyothibitisha Hasan al-Bannaa juu ya kipote chake yanaafikiana na madhehebu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au yanatofautiana nayo. Wacha tuangalie kutoka chini hadi juu. Ni yepi aliyothibitisha Hasan al-Bannaa katika ulinganizi na mfumo wake? Je, alikemea shirki kubwa inayofanywa katika nchi yake? Hapana. Je, alikemea Bid´ah na moja wapo kubwa ni Bid´ah ya Suufiyyah ambayo ni ya Wahdat-ul-Wujuud? Je, aliwakemea wenye nayo? Hapana. Badala yake alimsifu msudani al-Mirghaaniy as-Suufiy anayezungumza kwa Wahdat-ul-Wujuud. Wacha tutazame mfumo wake ulio na Bid´ah, shirki na mambo mengine ya kutisha.

Wacha tuangalie pia mfumo wa Jamaa´at-ut-Tabliygh. Je, wanalingania katika Tawhiyd? Je, wanaifanyia kazi Tawhiyd? Hapana. Uhakika wa mambo wanawakemea wale wanaolingania katika Tawhiyd.

Kunaweza kusemwa hayo hayo juu ya Suruuriyyah wanaoonelea kufaa kuwafanyia uasi viongozi na watawala wa waislamu.

Tukizingatia mifumo hii, tunaona kuwa wanafuata njia ya waumini au wanafuata njia ya isiyokuwa waumini? Hawafuati njia ya waumini kwa kuwa tunatambua kuwa njia ya waumini kunakusudiwa mfumo wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wale wenye kuwaiga katika Ahl-ul-Hadiyth ambao ni maimamu wa uongofu. Kupitia wao Allaah ameilinda dini Yake na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 04:115

[2] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 64-67
  • Imechapishwa: 27/01/2017