02. Ukweli wa shirki na kwamba mtazamo wa washirikina juu ya waungu wao

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Washirikina walikuwa wakiabudu kwenye masanamu hayo kwa sababu ya kutarajia baraka zao na kwamba yawaombee mbele ya Allaah. Hayo yameelezwa na Mola wetu pale aliposema:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[1]

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema:] “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”[2]

Hawakuwa wakiitakidi kuwa yanaumba na kuruzuku kama wanavyofikiria washirikina wa sasa. Wanadhani kwamba watu wale walikuwa wakiitakidi ya kwamba masanamu hayo yanaumba na kuruzuku. Walikuwa wakiona kuwa yameumbwa na ni yenye kuendeshwa na kwamba hayaumbi wala hayaruzuku. Lakini hata hivyo wanasema:

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema:] “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”

Pamoja na haya Allaah akawakufurisha, akawatumilizia Mtume na akawapiga vita kwa ajili ya shirki hii.

Haya yanambainishia msomaji ukweli wa shirki na kwamba ni kule kuwaomba uombezi waja wema, kuwaomba wamkurubishe mtu kwa Allaah, kuchinja kwa ajili yao, kuwawekea nadhiri na kuwasujudia kwa lengo la kujikurubisha na uombezi:

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”

وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“… na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”

Hawakusema kwamba wanaumba au wanaruzuku. Allaah ameyabainisha haya katika Kitabu Chake kitukufu pale aliposema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye hai na nani anayeendesha mambo?”  Watasema: “Ni Allaah.”[3]

Wao wanakubali kama alivosema (Ta´ala):

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.”[4]

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?” Bila shaka watasema: “Allaah.”[5]

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ

”Sema: ”Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo humo mkiwa mnajua?” Watasema: ”Ni ya Allaah.” Sema: ”Je, basi hamkumbuki?” Sema: ”Nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ‘Arshi kuu?” Watesema: ”Ni ya Allaah.” Sema: ”Je, basi kwa nini hamchi?” Sema: ”Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu, Naye ndiye alindaye na wala hakilindwi chochote kinyume Naye, ikiwa mnajua?” Watasema: ”Ni Allaah pekee.” Sema: ”Basi vipi mnazugwa?”

Kuna Aayah nyingi juu ya haya ambazo zote zinafahamisha ya kwamba Allaah ndiye Mwenye kuumba ardhi, Mwenye kuumba mbingu na kila kitu. Lakini hata hivyo walikufuru kwa ajili ya kuomba kwao uombezi, kujikurubisha kwa Mitume na waja wema, kuwachinjia, kuwawekea nadhiri na mfano wa hayo. Walikufuru kwa ajili ya haya. Vinginevyo wanajua kuwa viumbe wote Allaah ndiye kawaumba na ndiye Mwenye kuwaruzuku (Subhanaahu wa Ta´ala). Wao ni wenye kuyakubali hayo na hawana shaka yoyote. Lakini waliwafanya wakati na kati kwa sababu ya kutaka uombezi kutoka kwao, msamaha na mahitajio yao mengine. Walisema wazi kwamba wamejikurubisha kwao kwa sababu wanataraji uombezi wao na kwamba wawakurubishe. Ndipo Allaah akabainisha ubatilifu wa jambo hili na akabainisha kwamba kitendo hichi ni kufuru na upotevu na kwamba kule kuwaabudu kwao, kuwachinjia, kuwawekea nadhiri na kuwaomba yote ni katika shirki kubwa. Haijalishi kitu hata kama wanaonelea kuwa wameumbwa, ni wenye kuruzukiwa na Allaah, lakini midhali wamewafanyia ´ibaadah hizi, wakawataka uokozi, wakawawekea nadhiri, wakawachinjia, haya ndio shirki. Huenda watu hawa waliokuja nyuma wakitaka kweli kutia akilini basi watatia akilini, wakikumbushwa wataelewa kuhusu yale waliyokuwemo washirikina na kwamba haya wanayofanya ndio yaleyale waliyokuwa wakifuata washirikina wa kale.

[1] 10:18

[2] 39:03

[3] 10:31

[4] 43:87

[5] 39:38

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 10/08/2020