02. Sura ya pili: Vyanzo vya ´Aqiydah sahihi na mfumo wa Salaf katika kuipokea


´Aqiydah ni Tawqiyfiyyah. Haitakiwi kuthibitishwa isipokuwa kwa dalili kutoka katika Shari´ah. Hapa si pahala pa maoni wala Ijtihaad. Kwa ajili hiyo chanzo chake kimekomeka juu ya yale yaliyokuja katika Qur-aan na Sunnah. Kwa sababu hakuna yeyote ambaye ni mjuzi zaidi kuhusu Allaah, yaliyo ya wajibu kwake na aliyotakasika nayo kuliko Yeye Allaah Mwenyewe. Kama ambavyo hakuna yeyote, baada ya Allaah, ambaye ni mjuzi zaidi kuhusu Allaah kuliko Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo mfumo wa as-Salaf as-Swaalih na wale waliowafuata katika kuipokea ´Aqiydah ikawa umefupika juu ya Qur-aan na Sunnah. Yale yaliyofahamishwa na Qur-aan na Sunnah juu ya haki ya Allaah (Ta´ala) kinatakiwa kuaminiwa, kuitakidiwa na kutendewa kazi. Kile ambacho hakikufahamishwa na Qur-aan wala Sunnah basi Allaah (Ta´ala) ni mwenye kutakasika nacho na kukataliwa. Kwa ajili hiyo ndio maana hakukutokea tofauti kati yao katika ´Aqiydah. Uhakika wa mambo ni kuwa ´Aqiydah yao ilikuwa moja. Mkusanyiko wao ulikuwa mmoja. Allaah amechukua jukumu la kuwafanya wamoja wale wenye kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah, wakawa na ´Aqiydah sahihi na mfumo mmoja. Amesema (Ta´ala):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja na wala msifarikiane!”[1]

فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَىٰ

”Kisha utakapokufikieni kutoka Kwangu mwongozo, basi atakayeufuata mwongozo Wangu hatopotea na wala hatopata mashaka.”[2]

Kwa ajili hiyo ndio maana wakaitwa pote lililookoka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewashuhudia kuokoka pale alipokuwa akielezea kwamba Ummah utatofautiana katika makundi sabini na tatu na kwamba yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu. Pindi alipoulizwa juu ya hili moja akasema:

“Ni lile litalokuwa juu ya yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah wangu.”[3]

Hakika yametokea kweli yale aliyosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale baadhi ya watu walipozijenga I´tiqaad zao juu yale yasiyokuwa Qur-aan na Sunnah katika elimu ya falsafa, kanuni za mantiki zilizorithiwa kutoka kwa wanafalsafa wa kigiriki. Ndipo kukatokea upindaji na kutofautiana katika ´Aqiydah, mambo yaliyopelekea kutenganisha umoja, kufarikisha mkusanyiko na likabomolewa jengo la jamii ya kiislamu.

[1] 03:103

[2] 20:123

[3] at-Tirmidhiy (05/26).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 13/01/2020