1- Sifa ya kwanza: Harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Harufu hii ni yenye kuchukiza mbele za watu. Lakini mbele ya Allaah ni harufu nzuri zaidi kuliko harufu ya miski. Kwa sababu harufu hii imetokana na kumwabudu Allaah na kumtii. Kila chenye kutokana na kumwabudu na kumtii Yeye ni chenye kupendwa Kwake (Subhaanah) na Allaah humpa badali ambayo ni yenye kheri, bora na nzuri zaidi. Humuoni shahidi ambaye ameuliwa katika njia ya Allaah ambaye nia yake ni neno la Allaah liwe juu ambapo atakuja siku ya Qiyaamah na majeraha yake yanatoka damu, rangi yake ni rangi ya damu na harufu yake ni harufu ya miski? Katika hajj Allaah anajifakhari kwa Malaika juu ya wale wenye kusimama ´Arafah ambapo husema:

”Watazameni waja Wangu hawa ambao wamenijia wakiwa na nywele kemkem wakiwa na vumbi.”

Ameipokea Ahmad na Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake[1].

Nywele kemkem zimekuwa ni zenye kupendwa na Allaah katika hali kama hii kwa sababu ni jambo limetokana na kumtii Allaah kwa kujiepusha na mambo yaliyokatazwa wakati wa Ihraam na kuacha anasa.

[1] Ni Swahiyh kwa shawahidi zake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 09
  • Imechapishwa: 25/03/2020