02. Ni vipi kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan?


Ee waislamu! Hakika umekujieni mwezi mtukufu  na uliobarikiwa, nao si mwengine ni wa kufunga Ramadhaan. Ni mwezi ambao watu wanasimama usiku na kuswali. Katika mwezi huo wako ambao wanaachwa huru na Moto na wengine wanasamehewa madhambi. Katika mwezi huo watu hutoa swadaqah na kufanya matendo mema. Katika mwezi huo milango ya Pepo inafunguliwa na matendo mema yanalipwa zaidi na zaidi. Katika mwezi huo madhambi yanapungua. Du´aa zinaitikiwa. Watu wanapandishwa daraja. Madhambi yanasamehewa. Katika mwezi huo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) huwatunuku waja Wake neema mbalimbali na mawalii Wake hupata zawadi tele. Allaah amefanya kufunga mwezi huo ni moja katika nguzo za Uislamu. Mteuliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliufunga na akawaamrisha watu wafunge. Ameeleza kwamba yule ambaye ataufunga na kusimama nyusiku zake hali ya kuwa na imani na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah, basi Allaah atamsamehe madhambi yake yaliyotangulia. Katika mwezi huu kuna usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu moja. Atayenyimwa kheri zake kwa kweli huyo amenyima. Hivyo basi ukaribisheni – Allaah akurehemuni – kwa furaha na kuwa na maazimio ya kweli juu ya kuufunga, kuswali nyusiku zake na kushindana juu ya matendo mema.

Kimbia haraka sana kutubia juu ya madhambi na makosa yote. Peaneni nasaha na saidianeni juu ya wema na uchaji Allaah. Nasihianeni na amrishanane mema na mkatazane maovu na itaneni katika kheri zote ili muweze kupata Pepo na thawabu nyingi.

Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alikuwa akiwapa bishara njema Maswahabah zake juu ya kuja kwa mwezi wa Ramadhaan. Alikuwa akiwaeleza kuwa ndani [ya mwezi huu] milango ya rehema na Pepo hufunguliwa na vilevile milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa minyororo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Inapofika siku ya kwanza ya Ramadhaan mashaytwaan hufungwa minyororo na majini waovu hufungwa. Milango ya Moto hufungwa na hakuna unaofunguliwa na milango ya Pepo hufunguliwa na hakuna unaofungwa. Hunadi Mwenye kunadi: “Wewe unayetafuta kheri! Njoo! Wewe unayetafuta shari! Koma!” Kila usiku Allaah huwaacha huru watu fulani kutokamana na  Moto.”[1]

“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, mwezi wa baraka. Allaah huwafunikeni, huteremsha rehema, hufuta madhambi na huitikia du´aa ndani yake. Allaah hutazama namna mnavyoshindana ndani yake na hujifakhari kwenu mbele ya Malaika Zake. Kwa hivyo muonyesheni Allaah yale mazuri yenu. Hakika mla khasara ni yule mwenye kunyimwa rehema za Allaah.”[2]

Ee waislamu! Uchungeni mwezi huu mtukufu. Uadhimisheni – Allaah akurehemuni – kwa aina mbalimbali za ´ibaadah na matendo ya utiifu aina mbalimbali. Hakika ni mwezi mtukufu ambao Allaah ameufanya kuwa ni uwanja juu ya waja Wake. Ndani yake hushindana kwa utiifu na mema mbalimbali. Kwa hiyo kithirisheni – Allaah akurehemuni – kuswali, kutoa swadaqah, kuisoma Qur-aan kwa mazingatio na kuelewa, kusema “Subhaan Allaah”, “al-Hamdulillaah”, “Laa ilaaha illa Allaah”, “Allaahu Akbar”, Astaghfarullaah” na “Allaahumma swalli wa sallim ´alaa Muhammad” na watendeeni wema mafukara, masikini na mayatima. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mkarimu zaidi wa watu na katika Ramadhaan alikuwa ni mkarimu zaidi. Fuateni mwongozo wake – Allaah akurehemuni – na kuweni watoaji na wema zaidi. Tarajieni hesabu kwa Mfalme ambaye anajua kila kitu.

Hakikisheni mmezihifadhi swawm zenu kutokamana na yote yaliyoharamishwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ambaye haachi uongo, kuutendea kazi na ujinga, Allaah hana haja kuacha chakula chake na kinywaji chake.”[3]

“Swawm ni ngao. Mmoja wenu akifunga asiseme maneno ya upuuzi na wala kugombana. Mtu akimtukana aseme: “Nimefunga.””[4]

“Kufunga sio kule mtu kuacha chakula na kinywaji. Kufunga ni kujitenga mbali na upuuzi na maneno mabaya yote.”[5]

Ibn Hibbaan amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayefunga Ramadhaan na akatambua mipaka yake na akaihifadhi na yale yote yanayotakiwa kuhifadhiwa, atasamehewa madhambi yaliyo kabla yake.”[6]

Jaabir bin ´Abdillaah al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Ukifunga, unatakiwa vilevile kuzuia usikizi wako, uoni wako na ulimi wako kutokamana na uongo na ya haramu. Usimuudhi jirani. Swawm yako iwe na utulivu. Usizifanye siku zako ulizofunga kuwa kama masiku ambayo hukufunga.”

Ee waislamu! Swawm ni kitendo chema na kikubwa na thawabu zake ni tele na khaswa khaswa swawm ya Ramadhaan. Uadhimisheni – Allaah akurehemuni – kwa kuwa na nia njema na kujitahidi kuhifadhi swawm yake, kusimama nyusiku zake na kukimbilia matendo mema na kutubia madhambi na makosa yote. Tahadharini na yale Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walokataza na mtiini katika Ramadhaan na wakati mwingine. Usianeni na saidianeni juu ya hayo. Amrisheni mema na katazeni maovu ili muweze kupata Pepo, furaha, utukufu na kufuzu duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atutunuku kuweza kuufunga na kuswali nyusiku zake kwa kuamini na kutarajia malipo. Tunamuomba Allaah atujaalie sisi na waislamu wengine wote kuweza kuifahamu dini na kuifuata na atusalimishe sisi kutokamana na kile kinachosababisha hasira na adhabu Zake.

Tunamuomba Allah awawafikishe watawala na viongozi wa waislamu wote, azitengeneze hali zao na awafanye waweze kuhukumu kwa Shari´ah katika mambo yote kama ´ibaadah, matendo na mambo mengine yote. Tunamuomba Allaah awaongoze. Tunamuomba Allaah awaongoze katika hayo na watendee kazi:

وَأَنِ احْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ

“Wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Allaah.”[7]

أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ ۚوَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ

“Je, wanataka wahukumiwe hukumu ya kipindi cha kishirikina? Na nani mbora zaidi kuliko Allaah katika kuhukumu kwa watu wenye yakini [kwenye imani ndiye wenye kuyafahamu haya].”[8]

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Basi naapa kwa Mola wako hawatoamini mpaka wakufanye wewe kuwa ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kikamilifu kabisa.” (04:65)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wale wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni njia bora na matokeo mazuri zaidi.”[9]

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Na lile alilokupeni Mtume lichukueni na lile alilokukatazeni basi acheni.”[10]

Huu ndio uwajibu wa waislamu na viongozi wao wote. Ni wajibu kwa viongozi, wanachuoni wa waislamu na watu wa kawaida kumcha Allaah na kujisalimisha na Shari´ah Yake ilio na manufaa, uongofu na matokeo yenye kusifiwa. Kwayo kunafikiwa radhi za Allaah. Kwayo kunafikiwa haki iliyowekwa na Allaah. Kwayo kunaepukwa dhuluma.

Tunamuomba Allaah awatunuku mafanikio wote, awaongoze wote na awatunuku wote nia na matendo mema. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah wake.

[1] at-Tirmidhiy (682), Ibn Maajah (1642) na al-Haakim (1532). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy i ”Swahiyh-ul-Jaami´” (759).

[2] at-Twabaraaniy katika ”Musnad-ush-Shaamiyyiyn” (2238). Imezuliwa kwa mujibu wa al-Albaaniy  katika ”Dha´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (592).

[3] al-Bukhaariy (1903).

[4] al-Bukhaariy (1904) na Muslim (1151).

[5] al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (8096). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1082).

[6] Ahmad (11541) na Ibn Hibbaan (3433). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dha´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (584).

[7] 05:49

[8] 05:50

[9] 04:59

[10] 59:07