Pindi Uislamu ulipokuja ukamuondoshea dhuluma hizi kutoka kwa mwanamke na ukamrudishia yeye kuzingatiwa kama mtu. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke.”[1]

Ndipo (Subhaanah) akataja ya kwamba yeye ni mshirika wa mwanaume katika jambo la uutu kama ambavyo anashirikiana na mwanaume katika jambo la thawabu na adhabu juu ya matendo:

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mwenye kutenda mema katika wanamume au wanawake – ilihali ni muumini – basi Tutamhuisha maisha mazuri na Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.”[2]

Vilevile amesema (Ta´ala):

لِّيُعَذِّبَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ

“Ili Allaah awaadhibu wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike na washirikina wa kiume na washirikina wa kike.”[3]

Aidha Yeye (Subhaanah) akaharamisha kumzingatia mwanamke kuwa miongoni mwa mirathi ya mume inayorithiwa ambaye kishakufa. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَرِثُوا النِّسَاءَ كَرْهًا

“Enyi walioamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa kuwakirihisha.”[4]

Hivyo akamdhamini utu wake wenye kujitegemea na akamfanya kuwa ni mrithi na si mwenye kurithiwa, akamfanya mwanamke kuwa na haki ya kurithi kutoka katika mali ya ndugu yake. Amesema (Ta´ala):

لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ مِمَّا قَلَّ مِنْهُ أَوْ كَثُرَ ۚ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا

“Wanaume wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu na wanawake wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu – ikiwa ni kidogo au kingi; ni mgao uliofaridhishwa.”[5]

يُوصِيكُمُ اللَّـهُ فِي أَوْلَادِكُمْ ۖ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنثَيَيْنِ ۚ فَإِن كُنَّ نِسَاءً فَوْقَ اثْنَتَيْنِ فَلَهُنَّ ثُلُثَا مَا تَرَكَ ۖ وَإِن كَانَتْ وَاحِدَةً فَلَهَا النِّصْفُ

“Allaah anakuamrisheni kuhusu watoto wenu; mwanamume atastahiki mfano wa fungu la wanawake wawili na ikiwa wanawake ni zaidi ya wawili basi watastahiki theluthi mbili za alichokiacha. Lakini akiwa mtoto wa kike ni mmoja pekee basi atastahiki nusu.”[6]

Kuna mengine mengi yaliyotajwa juu ya mwanamke kurithi. Ni mmoja awe mama, msichana, dada na mke.

Katika upande wa uoaji Allaah akamfupizia mwanaume kuoa wanawake wane kwa sharti aweze kusimamia uadilifu unaowezwa baina ya wake. Amesema (Ta´ala):

فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً

“Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne.”[7]

Vilevile akawajibisha kuishi nao kwa wema. Amesema (Subhaanah):

وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Kaeni nao kwa wema.”[8]

Akafanya mahari ni haki yake na akaamrisha kumkadhibi nayo kikamilifu isipokuwa yale atakayoamua kuyasamehe kwa kuridhia kwake. Amesema:

وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً ۚ فَإِن طِبْنَ لَكُمْ عَن شَيْءٍ مِّنْهُ نَفْسًا فَكُلُوهُ هَنِيئًا مَّرِيئًا

“Wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa. Wakitoa chochote wenyewe katika mahari yao kwa kutaka kwao, basi kuleni kwa kufurahia.”[9]

Jengine Allaah akamfanya kuwa ni mchungaji, mwenye kuamrisha na kukataza ndani ya nyumba ya mume wake. Ni mwenye kuwaamrisha watoto zake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Mwanamke ni mchungi kwenye nyumba ya mume wake na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.”

Akamwamrisha mume kumuhudumia na kumpa mavazi kwa wema.

[1] 49:13

[2] 16:97

[3] 33:73

[4] 04:19

[5] 04:07

[6] 04:11

[7] 04:03

[8] 04:19

[9] 04:04

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 21/10/2019