02. Msimamo wa Salaf juu ya majina na sifa za Allaah

Madhehebu ya Salaf (Rahimahumu Allaah) yanahusiana na kuamini yale majina na zile sifa zote ambazo Allaah amejisifu Mwenyewe katika Qur-aan na yale majina na sifa zote ambazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemsifu kwayo. Wanayaamini hayo pasi na kuzidisha wala kupunguza, wala kuyavuka, kuyapindisha maana inayopingana na udhahiri wake wala kuyashabihisha na sifa za viumbe wala alama za mawazo. Bali wanayapitisha kama yalivyokuja na wakati huohuo wanarudisha elimu yake na maana yake kwa yale yaliyotajwa na kuzungumziwa.

Baadhi yao wameeleza ya kwamba Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Naamini yale yaliyotajwa kutoka kwa Allaah, kwa mujibu wa vile alivotaka Allaah, na ninaamini yale yaliyotajwa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa mujibu wa vile alivotaka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Walitambua kuwa yule aliyeyazungumza ni mkweli asiyekuwa na mashaka yoyote katika ukweli wake. Wakamsadikisha pamoja na kuwa hawajui uhakika wa namna yake. Hivyo wakawa wamenyamazia yale wasiyoyajua. Mambo yalikuwa hivo kwa karne na makarne. Wakausiana kufuata kwa wema na kusimama pale ziliposimama karne zengine. Wakatahadharisha juu ya kuvuka mfumo wao na kupinda kutoka katika njia yao. Wakabainisha mfumo na njia yao. Tunamuomba Allaah (Ta´ala) atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaowafuata.

Dalili inayoonyesha yale niyasemayo kuhusu madhehebu yao ni kwamba wao ndio wametunukulia Qur-aan tukufu na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ambayo hakuna mwengine anaweza kufanya hivo isipokuwa muumini. Waliyakubali pasi na kuyawekea mashaka wala wasiwasi kwa yule aliyeyasema. Hawakufasiri chochote kinachohusiana na sifa, hawakupindisha maana ya chochote wala hawakushabihisha na sifa za viumbe. Lau wangelifanya kitu katika hayo basi yangelitufikia. Haijuzu kuficha kitu kama hicho. Yale ambayo ni lazima kuyabainisha na kuyajua basi haifai kuyaficha. Walikokoteza sana juu ya kunyamazia jambo kama hilo, kiasi cha kwamba pindi mtu anapouliza juu ya kitu kisichokuwa wazi, walikuwa wanaweza kumkaripia kwa maneno makali yule muuliza, wakati mwingine kipigo na wakati mwingine kwa kumpuuza ili kumuonyesha machukizo ya yale aliyouliza.

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 9
  • Imechapishwa: 27/04/2018