02. Kulingania ni ´ibaadah tukufu

Kulingania kwa Allaah (Ta´ala) ni ´ibaadah tukufu ambayo Allaah ameamrisha, akahimiza na akawafanya watu wake ndio wenye maneno na matendo bora. Amesema (Ta´ala):

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

“Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania watu kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu?”[1]

Bi maana hakuna yeyote mwenye maneno bora kuliko yeye, kwa sababu amelingania kwa Allaah, ametendea kazi yale aliyolingania na akasema kwa kinywa kipana yale aliyomo pasi na kuona haya – bali amesema kuwa yeye ni katika waislamu. Haishangazi kuona mlinganizi amepanda katika ngazi hii, kwa sababu yeye ni mrithi wa Mitume katika kazi zao. Kazi yao ilikuwa kulingania kwa Allaah (Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amesema kumwambia wa mwisho na kiongozi wao:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[2]

Inafahamisha kuwa wafuasi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanalingania kwa Allaah (Ta´ala). Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema kuhusiana na Aayah hii:

”Amesema (Ta´ala) hali ya kumwamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awajuze watu na majini ya kwamba hii ndio njia yake, kwa msemo mwingine njia na mwenendo wake; kulingania kushuhudia kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika. Alinganie (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Allaah kwa utambuzi, yakini na hoja. Yeye na kila mwenye kumfuata alinganie katika yale anayolingania Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa utambuzi, yakini na hoja za kiakili na zilizowekwa katika Shari´ah.”[3]

[1] 41:33

[2] 12:108

[3] Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (2/744).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 7-8
  • Imechapishwa: 28/07/2022