02. Kosa la pili katika ´Aqiydah: Kuyafanya makaburi misikiti

2- Kuyafanya makaburi ni mahali pa kuswalia, kuswalia karibu nayo na kuweka makuba juu yake. Yote haya ni miongoni mwa njia za shirki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani mayahudi na wakristo juu ya jambo hilo na akatahadharisha jambo hilo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Allaah awalaani mayahudi na wakristo. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni sehemu ya kuswalia.”

Ameafikiana al-Bukhaariy na Muslim juu ya usahihi wake.

”Zindukeni! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakifanya makaburi ya Mitume wao na waja wao kuwa ni mahali pa kuswalia. Zindukeni! Msiyafanye kuwa ni mahala pa kuswalia. Hakika mimi nakukatazeni na jambo hilo.”

Ameipokea Muslim katika ”as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jundub. Muslim amepokea tena katika ”as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kulitia chokaa kaburi, kuliikalia na kulijengea.”

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Ni lazima kwa waislamu kujichunga na jambo hilo na wausiane kuliacha. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameonya juu ya jambo hilo. Isitoshe kitendo hicho ni njia inayopelekea kuwashirikisha wale waliyomo ndani ya makaburi, kuwaomba, kuwataka msaada, kuwaomba nusura na mengineyo katika aina mbalimbali za shirki.

Ni jambo linalotambulika kuwa shirki ndio dhambi aina kubwa kabisa, kabambe na yenye khatari zaidi. Kwa hiyo ni lazima kujichunga nayo na njia zake. Allaah amewaonya waja Wake kutokamana na hilo katika Aayah nyingi. Miongoni mwazo amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[2]

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha basi pasi na shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[3]

Zipo Aayah nyingi zikiwa na maana kama hii.

[1] 04:48

[2] 39:65

[3] 06:88

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Akhtwaau fiyl-´Aqiydah, uk. 2-3
  • Imechapishwa: 19/06/2020