02. Kazi ya Sunnah inapokuja katika Qur-aan

Mnatambua nyote ya kwamba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amemteua Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa utume Wake na akamkhusisha kwa ujumbe Wake. Amemteremshia Kitabu Chake kitukufu na akamwamrisha ndani yake kwa jumla yale aliyomwamrisha kwamba awabainishie nayo watu. Amesema (Ta´ala):

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao.” (16:44)

Naonelea kuwa ubainifu huu uliyotajwa katika Aayah hii tukufu umejumuisha bayana aina mbili:

Ya kwanza: Ubainifu wa matamshi na mpangilio. Huu ni ule ubalighisho wa Qur-aan na kutoificha na kuwafikishia nayo Ummah kama Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) alivyoiteremsha kwenye moyo wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya ndio makusudio ya maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ

“Ee Mtume! Fikisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako.” (05:67)

Vilevile mama ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) amesema:

“Atakayekuzungumzieni kuwa Muhammad ameficha kitu alichoamrishwa kufikisha, basi amemzulia Allaah uongo.” Halafu akasoma Aayah iliyotajwa.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Lau Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeficha kitu alichoamrishwa kufikisha, basi angeficha maneno (Ta´ala):

وَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِي أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَاتَّقِ اللَّـهَ وَتُخْفِي فِي نَفْسِكَ مَا اللَّـهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَاهُ

“Pale ulipomwambia ambaye Allaah amemneemesha nawe ukamneemesha: “Shikamana na mkeo na mche Allaah!” Ukaficha nafsini mwako aliyotaka Allaah kuyafichua nawe ukawaogopa watu ilihali Allaah ndiye ana haki zaidi ya kuogopwa.” (33:37)

Ya pili: Ubainifu wa maana ya matamko, sentesi au Aayah ambayo Ummah unahitajia kubainishiwa nayo. Mara nyingi hilo linakuwa katika Aayah za kijumla, zilizoenea na zilizoachiwa ambapo Sunnah inakuja na kuweka wazi zile Aayah za jumla, kuzifanya maalum zile zilizoenea na kuzifungamanisha zile zilizoachiwa. Hayo yanafanywa kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), matendo yake na kwa yale aliyoyakubali.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manzilat-us-Sunnah fiyl-Islaam, uk. 6-7
  • Imechapishwa: 10/02/2017