02. Jukumu maalum alopewa mwanadamu


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amemuumba mtu kwa neema Zake, akamtia sura tumboni mwa mama yake kwa hekima Yake, akamtoa nje kwa urafiki Wake na kumuwepesishia riziki Yake. Akamfunza yale ambayo alikuwa hayajui na akampa fadhilah kubwa. Akamjulisha juu ya alama za viumbe Wake na akamfanya kutokuwa na udhuru kupitia kwa Mitume ambao ndio viumbe bora kabisa. Akamwongoza amtakaye kutokana na fadhilah Zake na akampotosha ambaye amemtosa kutokana na hekima Yake. Amewafanyia wepesi waumini kwa ambayo ni mepesi na akavifungua vifua vyao kwa ajili ya ukumbusho. Wakamwamini Allaah hali ya kuwa ni wenye kutamka kwa ndimi zao na wenye kumtakasia nia kwa nyoyo zao. Wakatendea kazi yale waliyoletewa na Mitume Yake na kufikishwa na Vitabu Vyake. Wakajifunza yale Aliyowafunza, wakasimama pale Alipowawekea mpaka waliowekewa na wakaachana na wakatosheka na yale Aliyowahalalishia kutokamana na yale Aliyowaharamishia.

MAELEZO

al-Qayrawaaniy – Ni unasibisho wa mji huko magharibi mwa Afrika Qayrawaan. Mtunzi alikulia huko na akanasibishwa nako.

Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amemuumba mtu kwa neema Zake – Ameanza utangulizi huu kwa kumhimidi na kumsifu Allaah juu ya neema Zake tukufu. Miongoni mwazo ni kumuumba mwanadamu ambaye Allaah amemtilia umuhimu kwa kumuumba na kumtia sura. Kwa sababu kati ya viumbe wengine wote amemwandaa kwa jukumu kubwa, nalo ni kumwabudu Yeye pekee, hali ya kuwa hana mshirika. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[1]

Allaah amemtofautisha mtu huyu kwa sifa maalum zisizopatikana kwa viumbe wengine. Amemfanya kuweza kudhibiti vyote vilivyomo mbinguni na ardhini ili viweze kumsaidia kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Jalla wa ´Alaa) amemuumba mtu, akamfunza kuzungumza na akamruzuku aina mbalimbali za riziki yote hayo ili aweze kumwabudu Allaah (Jalla wa ´Alaa). Allaah alimuumba Aadam (´alayhis-Salaam), baba wa watu, na akamfanya kuwa ni khalifah ardhini. Akamfunza majina ya kila kitu na akamtukuza mbele ya Malaika kutokana na elimu. Mpaka wakakiri fadhilah zake. Baada ya kutofautiana kutokamana na wao kwa elimu akawaamrisha wamsujudie. Kwa sababu Aadam alijua kitu wasichokijua Malaika akawaamrisha wamsujudie sujudu ya kumsalimia na sio sujudu ya ´ibaadah. Sujudu ya ´ibaadah haijuzu kufanyiwa yeyote isipokuwa kwa Allaah (´Azza wa Jall). Hivo ndivo ilivyokuwa katika Shari´ah zote. Kuhusu sujudu ya kusalimia ni jambo lililokuwa linafaa katika Shari´ah zilizotangulia. Lakini hata hivyo katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) likafutwa. Kwa ajili hiyo haijuzu kumsujudia kiumbe, ni mamoja sujudu hiyo ni ya ´ibaadah au ni ya kusalimia. Sujudu ya Ya´quub na wanawake kwa Yuusuf ilikuwa ni sujudu ya maamkuzi na heshima, na si sujudu ya ´ibaadah.

[1] 51:56

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 11
  • Imechapishwa: 29/06/2021