02. Ibn Laadin Anawafurahisha Makafiri


Usaamah bin Laadin na wafuasi wake wanaeneza ufisadi katika ardhi kwa kuwaua watu ambao Uislamu haukuruhusu kuuawa. Wanaangamiza mali na pesa. Wanawatisha Waislamu na watu wengine ambao Shari´ah imewapa amani. Shari´ah haikuwapa idhini yoyote juu ya hilo. Akili iliyosalimika haikuwapa idhini yoyote juu ya hilo. Wamewafanya tu maadui wa Waislamu kufurahi. Wamewapa tu sababu ya kucheka. Wamewapa njia ili waweze kutukana ukubwa wa Uislamu na utukufu wa Waislamu wote. Waangamie! Ni ujasiri ulioje wameshikamana nao kwa jarima! Ni upupiaji ulioje walo nao juu ya maovu na madhambi!

Ibn Laadin amewapambia wapumbavu na wapuuzi wasiokuwa na uzowefu kujitoa muhanga. Kitendo hichi ni dhuluma na uadui. Matokeo yake wakaenda kujiua wao wenyewe na wengine ambao Shari´ah wala wenye busara haijaruhusu kuwaua miongoni mwa Waislamu na makafiri ambao wamepewa usalama na wana ahadi na Waislamu. Yule mwenye kuua watu sampuli hii basi amefanya dhambi ya kuangamiza. Mtu kama huyo anastahiki adhabu ilio kali kutokana na maandiko ya wazi na Hadiyth zilizo wazi. Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala) Amesema:

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

“Na atakayemuua muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni [Moto wa] Jahannam, ni mwenye kudumu humo na Allaah Atamghadhibikia na Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu.” (04:93)

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ أَن يَقْتُلَ مُؤْمِنًا إِلَّا خَطَأً ۚ وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَأً فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ وَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰ أَهْلِهِ إِلَّا أَن يَصَّدَّقُوا ۚ فَإِن كَانَ مِن قَوْمٍ عَدُوٍّ لَّكُمْ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ وَإِن كَانَ مِن قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ فَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰ أَهْلِهِ وَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ تَوْبَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا

“Na haiwi kwa muumini amuue muumini ila kwa kukosea tu. Na atakayemuua muumini kwa kukosea basi aachilie huru mtumwa muumini na atoe diya kwa kuisalimisha kwa watu wake [ahli wa maiti] isipokuwa watolee swadaqah [wasamehe haki yao]. Na ikiwa [muuliwaji] ni miongoni mwa watu wa maadui zenu ingawa naye ni muumini, basi [aliyeua] aachilie huru mtumwa muumini. Na ikiwa ni miongoni mwa watu ambao kuna mkataba baina yenu na baina yao, basi wapewe diya kuisalimisha kwa watu wake na aachiliwe huru mtumwa muumini. Asiyepata [au asiyekuwa na uwezo], afunge Swawm [badala yake] miezi miwili mfululizo; kuwa ni tawbah kwa Allaah. Na Allaah ni Mjuzi wa yote daima; Mwenye hikmah wa yote daima.” (04:92)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kumtukana Muislamu ni ufusaki [dhambi kubwa] na kumuua ni kufuru.” al-Bukhaariy (2995)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya kafiri ambaye Waislamu wana mkataba naye na mfano wake:

“Mwenye kumuua kafiri ambaye amepewa mkataba, basi hatonusa harufu ya Pepo. Harufu yake inapatikana sawa na umbali wa miaka arubaini.” al-Bukhaariy (2995).

Kwenye upokezi mwingine:

“… miaka sabini.” al-Haakim (2581).

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Harufu ya Pepo inapatikanaka sawa na umbali wa miaka mia moja. Hakuna mja mwenye kuiua nafsi ilio na mkataba isipokuwa Allaah Atamharamishia Pepo na harufu yake.” al-Haakim (2579) na Ahmad (05/46).

Abu Bakrah amesema:

“Allaah Anifanye kiziwi ikiwa sikumsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema hivo.”

Mtu huyu kutonusa harufu ya Pepo ina maana ya kwamba imeharamishwa kwake kwa muda Autakao Allaah. Mtu huyu yuko chini ya matakwa ya Allaah. Anafanya Alitakalo na Anahukumu Atakavyo.

Hii ndio hukumu ya Allaah na hukumu ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Aqiydah ya waumini katika suala hili.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Waqafaat wa Ma´aalim, uk. 8-10
  • Imechapishwa: 30/11/2014