Suala la pili: Hukumu ya kufunga Ramadhaan na dalili ya hilo:

Allaah (´Azza wa Jall) amefaradhisha kufunga mwezi wa Ramadhaan na akafanya ni moja katika nguzo zake tano. Hayo ni katika maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.”[1]

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo la batili. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”[2]

Pia kutokana na yale aliyopokea ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba kwa yule mwenye kuweza kuiendea.”[3]

Pia ni kutokana na yale aliyopokea Twalhah bin ´Ubaydillaah kwamba kuna mbedui mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa na nywele timtim akasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Ni nini alichonifaradhishia Allaah katika swawm?” Akasema: “Funga ya Ramadhaan.” Akauliza: “Je, kuna jengine linalonilazimu?” Akasema: “Hapana, isipokuwa kama utajitolea kitu… “[4]

Umamh umeafikiana juu ya ulazima wa kufunga Ramadhaan na kwamba ni moja katika nguzo za Uislamu ambazo zinatambulika kilazima katika dini na kwamba mwenye kuipinga ni kafiri na ameritadi nje ya Uislamu.

Kwa hivyo ulazima wa kufunga ukathibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Waislamu wameafikiana juu ya ukafiri wa mwenye kupinga.

[1] 02:183

[2] 02:185

[3] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[4] al-Bukhaariy (46) na Muslim (11).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 149-150
  • Imechapishwa: 13/04/2020