Tambua ya kwamba hatua hii kwa kiasi kikubwa inawahusu wazazi wawili. Wao ndio wanamlea mtoto, wanamfunza na wanamwelekeza katika manufaa yake. Hawatakiwi kuchoka kumpa malezi na kumfunza. Kumfunza mtoto udogoni ni kama kulichonga jiwe. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema pindi alipokuwa akiyafasiri maneno ya Allaah (Ta´ala):

قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ

“Jikingeni nafsi zenu na familia zenu na moto amabo kuni zake ni watu na mawe.”[1]

”Wafunzeni na wapeni adabu.”

Wazazi wanatakiwa kuwafunza watoto twahara, swalah na kuwachapa wasiposwali ilihali wameshafikisha miaka kumi. Wanatakiwa kumuhifadhisha mtoto Qur-aan, kumsikilizisha Hadiyth na kumfunza ile elimu anayoweza kuipokea katika miaka hiyo. Wanatakiwa kumfunza kuyaona mabaya vile vibaya na wamsisitize tabia njema. Wasichoke kumfunza yale anayoweza kuyapokea. Hakika hii ni hatua ya kupanda. Mshairi anasema:

Usitosheke na kumpa malezi mdogo
hata kama atalalama kuwa amechoka
Mwache mkubwa kama alivyo
ni mkubwa wa kupewa malezi

´Abdul-Malik bin Marwan alikuwa akimpenda mvulana wake al-Waliyd, lakini hamfunzi. Ikampelekea mwana yule kupatwa na utamkaji vibaya. ´Abdul-Malik akasema:

”Mapenzi yetu kwa al-Waliyd yamemdhuru.”

Mtoto anaweza kupata uelewa tangu utotoni mwake na akajichagulia mwenyewe njia. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ

“Hakika tangu hapo zamani [ujanani mwake] Tulikwishampa Ibraahiym uongofu [wa kuitambua njia ya haki] .”[2]

Imetajwa katika tafsiri za Qur-aan ya kwamba alikuwa mtoto wa miaka mitatu. Akaziambia nyota, mwezi na jua yale aliyoviambia mpaka alipofikia kusema:

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Hakika mimi nimeelekeza uso wangu, kwa imani safi na ya asli, kwa yule ambaye ameanzisha mbingu na ardhi, nami si katika washirikina.”[3]

Baada ya mtoto kufikisha miaka tano ndipo kunabainika uelewa na uchamgamfu wake katika mambo ya kheri. Uchaguzi wake mzuri unakuwa karibu na kipindi hichi. Anajitenga mbali na mambo mabaya na kinyume chake. ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alipita karibu na watoto waliokuwa wanacheza. Tahamaki walipomuona wote wakashika njia wakakimbia. Hakuna aliyebaki isipokuwa tu ´Abdullaah bin az-Zubayr (Radhiya Allaahu ´anh). Akamwambia: ”Kwa nini wewe hukukimbia?” Akajibu: ”Njia si yenye kiasi cha kwamba nihitaji kujitenga na sikufanya dhambi yoyote inifanye kuogopa.”

Khaliyfah al-Mu´taswim alimwambia mtoto wa waziri wake alipokuwa nyumbani kwao: “Ni nyumba ipi nzuri? Nyumba yetu au yenu?” Akajibu: “Nyumba yetu.” Ndipo khaliyfah akasema: “Kwa nini?” Mtoto yule akajibu: “Kwa kuwa wewe umekuja hapa.”

Uelewa wa mtoto na pia nguvu na udhaifu wa hima zake zinabaini kupitia zile chaguzi zake mwenyewe. Pindi watoto wanapokusanyika kwa ajili ya kucheza anasema yule mtoto aliye na hima yenye nguvu “Ni nani atakuwa pamoja na mimi?” ilihali yule mtoto aliye na hima dhaifu husema “Mimi nitakuwa pamoja na nani?” Wakati hima ya mtoto inapokuwa na nguvu huiacha elimu ndio itangulie mbele kabla ya kila kitu kingine.

Wakati mvulana anapokaribia kubaleghe basi inatakiwa kwa baba amuoze.

Ajabu ni kuwa baba haikumbuki hali yake mwenyewe pindi alipokuwa katika miaka hiyo na yale matatizo aliyokumbana nayo baada ya kubaleghe au kukawa vilevile kuna uwezekano alitumbukia katika kuteleza na akatambua kuwa mtoto wake ni kama yeye. Ibraahiym al-Harbiy amesema:

“Msingi wa kuharibika kwa watoto ni wao wenyewe kwa wenyewe.”

Sio wengi wanaoifanya elimu kutangulia mbele ya ndoa. Anatakiwa kujifunza kusubiri. Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) hakuoa isipokuwa baada ya kueneza miaka arubaini.

[1] 66:06

[2] 21:51

[3] 06:79

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin al-Jawziy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyh-un-Naa’im al-Ghamr ´alaa Mawswim-il-´Umr, uk. 47-54
  • Imechapishwa: 15/02/2017