Miongoni mwa mambo mlinganizi anatakiwa kulazimiana nayo ni kuwasahilishia watu wote na khaswa mahujaji. Masahilisho ni msingi miongoni mwa misingi ya Shari´ah. Haya ni muda wa kwamba hakuna andiko la wazi linalopingana na masahilisho hayo. Hata hivyo kukija andiko la wazi, haijuzu kupingana nalo kwa maoni. Huu ndio msimamo wa sawa na wa kati na kati ambao ni wajibu kwa kila mlinganizi kuufuata. Baada ya hapo vinapuuzwa vipingamizi vyote vya watu na maneno yao:

“Amefanya ugumu au wepesi?”

Kuna mambo mengi yenye kufaa ambayo baadhi ya watu wamezowea kuyaepuka kwa sababu ya fataawaa za baadhi ya watu zinazopingana na msingi ulioashiriwa punde tu. Naonelea kuyataja nayo ni kama yafuatayo:

1- Kuoga, japokuwa kwa kusugua kichwa, hata kama ni pasi na kuota. Hilo limethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na ya Muslim na nyenginezo kutokana na Hadiyth ya Abu Ayyuub (Radhiya Allaahu ´anh)[1].

2- Kujikuna kichwa ijapo zitaporomoka baadhi ya nywele. Dalili ya hilo ni Hadiyth ya Abu Ayyuub niliyoiashiria punde tu. Hayo ndio maoni yaliyochaguliwa na Shaykh-ul-Islaam ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah).

3- Kufanya chuku, ijapo itapelekea kunyoa ile sehemu ya kufanya chuku. Alifanya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) chuku katikati ya kichwa chake na hali ya kuwa ni mwenye kufanya Ihraam. Kitendo hichi hakiwezi kufanyika isipokuwa kwa kunyoa baadhi ya nywele. Haya nido maoni ya Ibn Taymiyyah. Pia Hanaabilah wanafuata maoni haya lakini wamemuwajibishia mwenye kufanya hivo kutoa fidia, jambo wasilokuwa nalo dalili.  Bali maoni yao ni yenye kurudishwa kwa kupiga kwake chuku (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lau angelikuwa ametoa fidia, basi mpokezi angelitaja. Kutaja kwake kufanya chuku bila ya fidia, ni dalili ya kwamba hakukupatikana fidia. Kwa hivyo maoni ya sawa ni ya Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah).

4- Kunusa harufu nzuri na kuondoa kucha iliyovunjika. Katika hilo kuna mapokezi yaliyotajwa katika “msingi”.

5- Kutafuta kivuli kwenye hema au chini ya nguo. Hilo limethibiti kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mfano wake mtu hapo kabla alikuwa akitafuta kivuli cha kipando. Leo mtu anaweza kufanya hivo kwa mwanvuli au hata ndani ya gari. Kuwajibisha kutoa fidia kwa sababu ya hilo ni kutilia uzito kusikokuwa na dalili. Maoni sahihi ni kuwa hayatofautishi kati ya kutafuta kivuli kwenye hema, jambo ambalo limethibiti katika Sunnah, na kutafuta kivuli kwenye kipando na vitu mfano wake. Huo ni upokezi mmoja kutoka kwa Imaam Ahmad kama ilivyokuja katika “Manaar-us-Sabiyl” (01/236). Kuna makundi yanayoondosha sakafu ya gari na hilo si jengine isipokuwa ni kupetuka mipaka katika dini, jambo ambalo halikuidhinishwa na Mola wa viumbe.

6- Kufunga mshipi na mkanda kwneye Izaar. Inafaa kuufunga wakati wa haja. Kadhalika inafaa kuvaa pete, kama ilivyokuja katika baadhi ya mapokezi. Vilevile inafaa kuvaa saa, miwani na pochi ya pesa shingoni.

Mambo yote haya yanaingia kwenye ule msingi uliotajwa. Baadhi yake yanatiliwa nguvu na Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mapokezi kutoka kwa Maswahabah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Allaah anakutakieni mepesi na wala hakutakieni magumu.”[2]

Na himdi zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] Hadiyth yote imetajwa katika “msingi”, uk. 28. Nimeitaja katika “al-Irwaa´-ul-Ghaliyl” (1019) na “Swahiyh Abiy Daawuud” (1613).

[2] 02:185

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 13/08/2017