Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akuogoze katika kumtii – ya kwamba Haniyfiyyah ni dini ya Ibraahiym, nayo ni kumwabudu Allaah peke yake hali ya kuwa ni mwenye kumtakasia Yeye dini. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

MAELEZO

Tambua – Allaah akuogoze katika kumtii… “

Hii ni du´aa kutoka kwa Shaykh (Rahimahu Allaah). Namna hii inatakiwa kwa mwalimu amuombee du´aa mwanafunzi.

Kumtii Allaah maana yake ni kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake.

“… ya kwamba Haniyfiyyah ni dini ya Ibraahiym… “

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amemuamrisha Mtume wetu kufuata mila ya Ibraahiym. Amesema (Ta´ala):

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba ufuate mila ya Ibraahiym inayojiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd na hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:123)

Haniyfiyyah ni upwekeshaji ambayo ndio dini ya Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). “Haniyf” ni yule mwenye kumuelekea Allaah na kuvipa mgongo vyengine vyote. Hii ndio maana ya “Haniyf”; ni yule mwenye kumuelekea Allaah kwa moyo wake, matendo yake, nia na makusudio. Vyote atekelezewe Allaah. Upande mwingine amevipa mgongo vyengine vyote. Allaah ametuamrisha kufuata dini ya Ibraahiym:

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ

“Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika dini. Mila ya baba yenu Ibraahiym.” (22:78)

Dini ya Ibraahiym ni kumwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini. Hii ndio Haniyfiyyah. Hakusema kumwabudu Allaah peke yake, pasi na Ikhlaasw. Hii ina maana ya kwamba unatakiwa kujiepusha na shirki, kwa sababu ´ibaadah ikichanganyika na shirki inabatilika. Haiwi ´ibaadah isipokuwa pale itapokuwa ni yenye kusalimika na shirki aina zote kubwa na ndogo. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini kwa kujiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd.” (98:05)

“Haniyf” ni yule mwenye kuelekea kwa Allaah (´Azza wa Jall) kitakasifu.

Allaah kawaamrisha ´ibaadah hii viumbe wote. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”

Maana ya ´waniabudu` ni kwamba wanipwekeshe kwa ´ibaadah. Hekima ya kuumbwa viumbe ni wamwabudu Allaah (´Azza wa Jall) hali ya kumtakasia Yeye dini. Kuna baadhi walijisalimisha na ambapo wengine hawakufanya hivo. Lakini hii ndio hekima ya kuumbwa kwao. Anayemuabudu mwengine asiyekuwa Allaah, anaenda kinyume na hekima ya kuumbwa viumbe na vivyo hivyo anaenda kinyume na maumbile na Shari´ah.

Ibraahiym ndiye baba wa Mitume waliokuja baada yake. Wote ni katika kizazi chake. Ndio maana amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِ النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ

“Tukajaalia katika dhuria yake Unabii na Kitabu.” (29:27)

Wajukuu wote wa Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) ni wana wa Israaiyl isipokuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kutoka katika kizazi cha Ismaa´iyl. Kwa hivyo Mitume yote wanatokamana na Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) ikiwa ni heshima kwake. Allaah alimfanya kuwa ni kiongozi wa watu, bi maana kiigizo chema:

قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا

“Akasema: “Hakika Mimi nakufanya uwe ni kiigizo kwa watu.”” (02:124)

إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً

“Hakika Ibraahiym alikuwa ni kiigizo.” (16:120)

Bi maana kiigizo wa kuigwa. Haya Allaah amewaamrisha viumbe wote. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”

Ibraahiym aliwaita watu kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall), kama walivyofanya Mitume wengine wote. Mitume wote waliwaita watu kumwabudu Allaah peke yake na kutomwabudu mwengine yeyote. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [kila chenye kuabudiwa asiyekuwa Allaah].”” (16:36)

Kuhusu Shari´ah ambayo ni maamrisho, makatazo, ya halali na ya haramu, inatofautiana kwa kutofautiana kwa nyumati kwa mujibu wa haja na mahitajio yao. Allaah anaweka Shari´ah kisha baadaye anaifuta kwa kuweka Shari´ah nyingine. Hali iliendelea kuwa hivo mpaka kulipokuja Shari´ah ya Uislamu ikafuta Shari´ah zengine zote. Shari´ah hii itaendelea kubaki mpaka Qiyaamah kisimame. Kuhusu msingi wa dini ya Mitume, ambayo ni Tawhiyd, unabaki, haufutwi na wala haufuti. Dini yao ni moja ambayo ni Uislamu, maana yake ni kumtakasia nia Allaah, kumwabudu Allaah yekee. Shari´ah zinaweza kutofautiana na kufutwa, lakini Tawhiyd na ´Aqiydah ni moja kuanzia kwa Aadam mpaka kwa Mtume wa mwisho. Wote walikuwa wakiita katika Tawhiyd na kumwabudu Allaah peke yake. Kumwabudu Allaah ni kutii maamrisho ya Shari´ah Yake. Shari´ah hii ikifutwa, ´ibaadah inakuwa kwa kutendea kazi yale yaliyofuta na kutendea kazi yale yaliyofutwa hayazingatiwi tena kuwa ni kumwabudu Allaah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 18/08/2022