Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

671- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Mkiuona fungeni na mkiuona fungueni. Mkifunikwa na mawingu basi ikadirieni.”[1]

 Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Mkifunikwa na mawingu, basi ikadirieni siku thelathini.”[2]

Katika upokezi wa al-Bukhaariy imekuja:

“Mkifunikwa na mawingu, basi kamilisheni idadi ya siku thelathini.”[3]

672- Amepokea pia kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“… mkamilishe idadi ya Sha´baan siku thelathini.”[4]

673- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Watu waliona mwezi mwandamo. Nikamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba nimeuona ambapo akafunga na akawaamrisha watu kufunga.”[5]

Ameipokea Abu Daawuud. Ameisahihisha Ibn Hibbaan na al-Haakim.

674- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba kuna mbedui mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema:

“Mimi nimeuona mwezi mwandamo. Akasema: “Wewe unashuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Ndio.” Akamuuliza tena: “Unashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ndio.” Ndipo akasema: “Ee Bilaal! Watangazie watu wafunge kesho!”[6]

Wameipokea watano na akaisahihisha Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan. an-Nasaa´iy ameonelea kuwa kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi[7].

MAELEZO

Hadiyth hizi zinafahamisha kuanza kwa Ramadhaan kunathibiti kwa ushahidi wa mtu mmoja. Ibn ´Umar amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Mkiuona fungeni na mkiuona fungueni. Mkifunikwa na mawingu basi ikadirieni.”

Pia (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza namna alivyoona mwezi mwandamo ambapo akamweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafunga yeye na akawaamrisha watu wengine nao kufunga. Mtu mkweli, mwaminifu na mwenye uoni mkali akishuhudia kwamba ameona mwezi mwandamo, basi inathibiti kuingia kwa mwezi kwa ushahidi wake. Kuhusu kuisha kwa mwezi wa Ramadhaan ni jambo halithibiti isipokuwa kwa ushahidi wa watu wawili. Hilo ni kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wakishuhudia mashahidi wawili fungeni na fungueni.”[8]

Serikali yetu imechukua njia salama ya hali ya juu kuhusiana na suala hili. Hivyo mwezi ukithibiti kuingia au kuisha kupitia vyombo vya mawasiliano vya Saudia, basi ni lazima kutendea kazi.

[1] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (1080).

[2] Muslim (1081).

[3] al-Bukhaariy (1907).

[4] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (1081).

[5] Abu Daawuud (2342), Ibn Hibbaan (3447) na al-Haakim (1/423).

[6] Abu Daawuud (2340), at-Tirmidhiy (691), an-Nasaa’iy (2112), Ibn Maajah (1652), Ibn Khuzaymah (1923), Ibn Hibbaan (3446) na ad-Daarimiy (1692). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (907).

[7] as-Sunan al-Kubraa (3/99).

[8] an-Nasaa’iy (2116).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/406-409)
  • Imechapishwa: 23/04/2020