Swali 2: Wakati wa kiangazi kunachezwa maigizo na Anaashiyd. Ni yepi maoni yako juu ya hilo?

Jibu: Ni wajibu kwa wasimamizi wa vituo vya kiangazi kusitisha vitu vyote visivyokuwa na faida au vyenye madhara kwa wanafunzi. Wawafunze Qur-aan, Sunnah, Hadiyth, Fiqh na lugha ya kiarabu. Haya yanatosha na kumfanya mtu kutokuwa na wakati wa mambo mengine. Wanatakiwa kuwafunza pia elimu ambayo itakuja kuwanufaisha katika dunia kama mfano wa kuandika, hesabu na ujuzi wenye faida. Kuhusu mambo yanayoitwa “burudani” hayatakiwi kuwepo katika barnamiji[1]. Yanapoteza wakati. Pengine hata yakawashughulisha na kuwasahaulisha lile lengo lililowaleta. Miongoni mwa mambo hayo ni uigizaji na Anaashiyd. Haya si jengine isipokuwa ni pumbao na mchezo. Ukiongezea juu ya hilo yanawafanya wanafunzi kuangalia michezo ya kuigiza na kusikiliza nyimbo zinazorushwa katika vyombo mbalimbali vya khabari.

[1] Shaykh Swaalih al-Fawzaan amesema:

“Kitu ambacho inatakikana kukizindua ni yale ambayo vijana wengi wenye dini wametumbukia ndani yake. Wanasikiliza Anaashiyd zinazoimbwa kwa sauti za pamoja na wanaziita kuwa ni “Anaashiyd za Kiislamu”. Ni aina ya nyimbo na wakati mwingine zinaimbwa kwa sauti zenye kufitinisha. Kanda hizi zinauzwa pamoja na kanda za Qur-aan tukufu na mihadhara ya dini. Anaashiyd hizi kuziita kuwa ni “Anaashiyd za dini” ni makosa. Kwa sababu Uislamu haukutuwekea Sharii´ah ya Anaashiyd. Kinyume chake umetuwekea Shari´ah ya kumdhukuru Allaah, kusoma Qur-aan, kujifunza elimu yenye manufaa na mengineyo.

Kuhusiana na Anaashiyd ni katika dini ya Suufiyyah iliyozushwa. Wameifanya dini kuwa ni pumbao na mchezo. Kuzifanya Anaashiyd ni katika dini ni jambo limeshabihiana na manaswara ambao dini yao wameifanya nyimbo na sauti za pamoja.

Lililo la wajibu ni kutahadhari na Anaashiyd hizi na kupiga marufuku kuuzwa na kusambazwa. Isitoshe Anaashiyd hizi zinaweza kuchochea katika hamasa zenye fitina na uchochezi kati ya waislamu.

Wanaeneza Anaashiyd hizi kwa kutumia hoja ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati fulani alikuwa anasomewa mashairi na akasikiliza na kuzikubali. Jibu ya hilo ni kwamba mashairi yaliyokuwa yakisomwa mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayakuwa yanasomwa kwa sauti za pamoja kwa sampuli ya nyimbo. Vilevile hayakuwa yanaitwa “Anaashiyd za Kiislamu”. Ilikuwa ni mashairi ya kiarabu ambayo ndani yake kuna hekima, methali, ujasiri na ukarimu. Maswahabah walikuwa kila mmoja akiyasoma kivyake kutokana na maana yaliyokuwa nayo. Walikuwa wanaweza kusoma mashairi wakati wanapofanya kazi za nguvu kama ya ujenzi au safari za usiku. Ni dalili inayoonyesha kuwa yameruhusiwa mambo kama hayo katika hali kama hizo, sio kuyafanya kuwa ni sanaa katika kulea na kulingania, kama inavyofanywa leo pindi wanafunzi wanapojifunza Anaashiyd hizi na kuziita kuwa ni “Anaashiyd za Kiislamu” au “Anaashiyd za kidini”. Hii ni Bid´ah katika dini na zinatoka katika dini ya Suufiyyah iliyozushwa. Wao ndio wenye kutambulika kufanya Anaashiyd kuwa ni kipengele cha dini.

Ni wajibu kuzindua kampeni hizi na kupiga marufuku kuuzwa kanda hizi. Kwa sababu shari huanza kidogo kidogo. Ikiwa mtu hakuichukulia hatua mapema zitakuja kuendelea na kukua.” (al-Khutwab al-Minbariyyah (03/184-185)

Muheshimiwa Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn aliulizwa kuhusu Anaashiyd za Kiislamu. Hapa chini kunafuatia swali na jibu:

Swali: Je, inajuzu kwa wanaume kuimba Anaashiyd za Kiislamu? Je, inajuzu kuwapigia dufu wanapoimba? Je, inajuzu kuimba Anaashiyd mbali na sikukuu na sherehe?

Jibu: Anaashiyd za Kiislamu ni Anaashiyd zilizozushwa. Zimeshabihiana na waliyozusha Suufiyyah. Kwa hivyo inatakiwa kwa mtu kujitenga nazo mbali na badala yake afuatilie mawaidha ya Qur-aan na Sunnah. Isipokuwa tu labda katika vita ili ziweze kusaidia kuleta motisha na jihaad katika njia ya Allaah (Ta´ala). Ni jambo zuri. Anaashiyd zikiambatana na dufu basi zinakuwa mbali zaidi na usawa. (Fataawaa ash-Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn (01/134-135))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 08/10/2016