02. Dalili za uwajibu wa kuifuata Qur-aan

Msingi wa kwanza: Kitabu kitukufu cha Allaah. Maneno ya Mola wetu (´Azza wa Jall) sehemu nyingi katika Qur-aan zimeonyesha kuwa ni wajibu kufuata Kitabu hichi na kushikamana nacho na vilevile kusimama kwenye mipaka yake. Amesema (Ta´ala):

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu na wala msifuate badala Yake walinzi; ni machache mnayoyakumbuka.” (07:03)

وَهَـٰذَا كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ فَاتَّبِعُوهُ وَاتَّقُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Na hiki Kitabu Tumekiteremsha kilichobarikiwa, basi kifuateni na muche ili mpate kurehemewa.” (06:155)

قَدْ جَاءَكُمْ رَسُولُنَا يُبَيِّنُ لَكُمْ كَثِيرًا مِّمَّا كُنتُمْ تُخْفُونَ مِنَ الْكِتَابِ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ ۚ قَدْ جَاءَكُم مِّنَ اللَّـهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ يَهْدِي بِهِ اللَّـهُ مَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَهُ سُبُلَ السَّلَامِ وَيُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِهِ وَيَهْدِيهِمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Hakika amekujieni Mtume wetu ambaye anakubainishieni mengi katika yale mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu na anasamehe mengi. Hakika imekujieni kutoka kwa Allaah nuru na Kitabu kinachobainisha; Allaah kwacho anamwongoza yule atakayefuata radhi Zake katika njia za salama na anawatoa katika viza kuingia katika nuru kwa idhini Yake na anawaongoza katika njia iliyonyooka.” (05:15-16)

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖوَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ

”Hakika wale waliokanusha Ukumbusho ulipowajia na hakika hicho ni Kitabu chenye utukufu; hakiingiliwi na batili mbele yake na wala nyuma yake. Ni uteremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima, Mwenye kuhimidiwa.” (41:41-42)

قُلْ أَيُّ شَيْءٍ أَكْبَرُ شَهَادَةً ۖ قُلِ اللَّـهُ ۖشَهِيدٌ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۚ وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ

“Sema: “Ni kitu gani ushahidi wake ni mkubwa kabisa?” Sema: “Allaah, Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itayemfikia.” (06:19)

هَـٰذَا بَلَاغٌ لِّلنَّاسِ وَلِيُنذَرُوا بِهِ

“Huu ni ufikisho kwa watu na ili wawaonye kwayo.” (14:52)

Kuna Aayah nyingi zilizo na maana kama hii.

Kumekuja vilevile Hadiyth nyingi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zikiamrisha kushikamana barabara na Qur-aan. Zimefahamisha kuwa mwenye kushikamana nayo yuko juu ya uongofu na mwenye kukiacha yumo upotevuni. Miongoni mwa hayo ni yale yaliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alisema katika Khutbah yake katika hajj ya kuaga:

“Mimi nimekuachieni kile ambacho iwapo mtashikamana nacho basi hamtopotea: Kitabu cha Allaah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake tena kupitia kwa Zayd bin Arqam (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi nimekuachieni vizito viwili ambapo cha kwanza ni Kitabu cha Allaah. Ndani yake mna uongofu na nuru. Hivyo basi, chukueni Kitabu cha Allaah na shikamaneni nacho.”

Akasisitiza na kukokoteza juu ya Kitabu cha Allaah. Kisha akasema:

“… na watu wa familia yangu. Ninakukumbusheni Allaah juu ya watu wa familia yangu. Ninakukumbusheni Allaah juu ya watu wa familia yangu.”

Katika upokezi mwingine amesema kuhusu Qur-aan:

“Ni kamba ya Allaah. Mwenye kushikamana nayo atakuwa juu ya uongofu na mwenye kuiacha atakuwa juu ya upotevu.”

Hadiyth zilizo na maana kama hii ni nyingi.

Kuna maafikiano ya wanachuoni na watu wa imani katika Maswahabah na waliokuja baada yao juu ya kushikamana na Qur-aan, kuhukumiwa nayo na kuhukumiana nayo pamoja na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakutotosha kurefusha kutaja dalili zilizothibtii juu ya suala hili.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ujuwb-ul-´Amal bis-Sunnah
  • Imechapishwa: 23/10/2016