02. Dalili katika Qur-aan kuacha swalah ni ukafiri mkubwa

Allaah (Ta´ala) amesema katika Suurah “at-Tawbah”:

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ

“Wakitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi ni ndugu zenu katika dini.”[1]

Amesema (Ta´ala) katika Suurah “Maryam”:

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ وَلَا يُظْلَمُونَ شَيْئًا

“Baada yao wakaja watu waovu. Walipoteza swalah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu kali. Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda mema, basi hao wataingia Peponi na wala hawatadhulumiwa kitu.”[2]

Dalili katika Suurah “Maryam” ni pale Allaah anaposema kuhusiana na wale wenye kuipuuza swalah na kufuata matamanio yao:

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا

“Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda mema.”

Ni dalili inafahamisha kuwa walipoipuuza swalah na wakafuata matamanio yao wakawa sio waumini.

Dalili katika Suurah “at-Tawbah” ni kwamba Allaah (Ta´ala) ameweka masharti matatu ya udugu kati yetu na washirikina:

1- Watubie juu ya shirki.

2- Wasimamishe swalah.

3- Watoe zakaah.

Wakitubu juu ya shirki na wasiswali na wala wasitoe zakaah, sio ndugu zetu. Vilevile ikiwa wataswali na wasitoe zakaah sio ndugu zetu. Udugu wa dini haukatiki isipokuwa pale ambapo mtu atatoka katika dini kabisa kabisa. Haukatiki kwa sababu ya dhambi kubwa wala kufuru ndogo. Huoni namna ambavyo Allaah (Ta´ala) amethibitisha kuwa muuaji ni ndugu wa yule muuliwaji pale aliposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِصَاصُ فِي الْقَتْلَى ۖ الْحُرُّ بِالْحُرِّ وَالْعَبْدُ بِالْعَبْدِ وَالْأُنثَىٰ بِالْأُنثَىٰ ۚ فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa kisasi waliouawa: muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa ihsani.”[3]

Pamoja na kwamba kuua kwa kukusudia ni dhambi kubwa kabisa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

“Atakayemuua muumini kwa kusudi, basi malipo yake ni Moto, ni mwenye kubaki humo kwa muda mrefu; na Allaah atamghadhibikia na atamlaani na atamuandalia adhabu kuu.”[4]

Huoni alivyosema Allaah (Ta´ala) kuhusu makundi mawili ya waumini yanapopigana vita:

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Ikiwa makundi mawili ya waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao, lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni vita na lile ambalo linakandamiza mpaka lielemee katika amri ya Allaah; likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu na fanyeni haki. Hakika Allaah anapenda wafanyao haki. Hakika waumini ni ndugu. Suluhisheni baina ya ndugu zenu [waliotofautiana] na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.”?[5]

Allaah (Ta´ala) amethibitisha udugu kati ya kundi lenye kusuluhisha na makundi mawili yenye kupigana vita. Pamoja na kuwa kumpiga vita muislamu ni kufuru. al-Bukhaariy na wengine wamepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumpiga vita ni kufuru.”[6]

Lakini aina ya kufuru hii ni ile isiyomtoa mtu katika Uislamu. Ingelikuwa ni kufuru yenye kumtoa mtu katika Uislamu basi kusingelibaki udugu wa kiimani. Aayah tukufu imethibitisha kuwa udugu wa imani unabaki pamoja na kuwa wanapigana vita.

Kwa haya inapata kujulikana kuwa kuacha swalah ni ukafiri mkubwa unaomtoa mtu katika Uislamu. Kwa sababu lau kuacha swalah ingelikuwa ni dhambi nzito au kufuru ndogo tu basi udugu wa kidini usingekatika, kama jinsi haukatiki vilevile kwa kumuua na kumpiga vita muumini.

Endapo mtu atauliza kama tunamkufurisha yule ambaye hatoi zakaah, kama inavyoweza kufahamika katika Suurah “at-Tawbah”, tunasema kuwa kuna baadhi ya wanachuoni wenye kuonelea hivo. Ni moja kati ya maoni mawili ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Hata hivyo naonelea kuwa maoni yenye nguvu ni kuwa hakufuru. Pamoja na hivyo ataadhibiwa adhabu kubwa, kitu ambacho kimetajwa na Allaah (Ta´ala) katika Kitabu Chake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Sunnah yake. Moja wapo ni yale aliyopokea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusiana na adhabu ya yule asiyetoa zakaah:

“Hatimae ataona njia yake; ima ya kuelekea Peponi au ya kuelekea Motoni.”[7]

Inafahamisha kuwa hakufuru. Kwa sababu angelikuwa ni kafiri kusingelikuwa na uwezekano wa kuingia Peponi. Hivyo tamko la Hadiyth hili linakuwa ni lenye kutangulia mbele ya kile chenye kueleweka katika Aayah. Ni jambo linalojulikana katika kanuni ya kwamba tamko linatangulia mbele ya kile kinachoeleweka.

[1] 09:11

[2] 19:59-60

[3] 02:178

[4][4] 04:93

[5] 49:09-10

[6] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

[7] Muslim (987).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 4-6
  • Imechapishwa: 22/10/2016