02. Baadhi ya Hadiyth kuhusu kuishi Shaam

1- ´Abdullaah bin Hawaalah amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mambo yataishilia maaskari watakuwa ni wenye kushikamana: wanajeshi wa Shaam, wanajeshi wa Yemen na wanajeshi wa Iraq.” Ibn Hawaalah akasema: ”Nijiunge na kina nani, ee Mtume wa Allaah, endapo nitakutana na hayo?” Akasema: ”Shikamana na Shaam kwani hakika ndio ardhi bora ya Allaah.” Huko Allaah huwateua waja Wake bora. Iwapo mtakataa basi chagueni Yemen na kunyweni kutoka chemchem yake. Hakika Allaah amechukua jukumu juu yangu la kuiangalia Shaam na watu wake.”

Ameipokea Imaam Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake na al-Haakim ambaye amesema:

”Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.”

Abu Haatim ar-Raaziy amesema:

“Hadiyth ni Swahiyh, nzuri na geni.”

Imepokelewa kwa njia nyingi. Nimezitaja katika “Sharh at-Tirmidhiy”.

2- Imaam Ahmad, at-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kutajitokeza moto Hadhramawt ambao utawafukuza watu.” Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unatuamrisha nini?” Akasema: “Shikamaneni na Shaam.”

Ni Swahiyh kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

3- Imaam Ahmad na at-Tirmidhiy wamepokea kupitia kwa Bahz bin Hakiym ambaye ameeleza ya kwamba alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Unatuamrisha wapi?” Akasema: “Hapa!” Akaashiria Shaam kwa mkono wake na kusema: “Hakika nyinyi mtakusanywa kwa miguu na kwa kupanda kipando na mtaachwa juu ya nyuso zenu.”

Katika upokezi wa Imaam Ahmad imekuja:

“Akaashiria Shaam kwa mkono wake na kusema: “Pale ndipo mtakusanywa.”

Ameisahihisha vilevile at-Tirmidhiy.

4- Imaam Ahmad amepokea kupitia kwa Abu Umaamah al-Baahiliy ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jilazimieni na Shaam.”

5- Imaam Ahmad amepokea kupitia kwa Abu Dharr aliyesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafanya nini ukifukuzwa kutoka al-Madiynah?” Nikasema: “Basi nitaishi kwa raha na amani na kwenda zangu na kuwa njiwa katika njiwa za Makkah.” Ndipo akasema: “Utafanya nini ukifukuzwa kutoka Makkah?” Nikasema: “Basi nitaishi kwa raha na amani na kwenda zangu Shaam na ardhi Takatifu.” Akasema: “Utafanya nini ukifukuzwa kutoka Shaam?” Nikasema: “Ninaapa kwa Yule aliyekutuma kwa haki ya kwamba nitauweka upanga wangu juu ya bega langu.” Akasema: “Au kilicho bora kuliko hicho? Sikiliza na utii hata kama atakuwa mja wa kihabeshi.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 02/02/2017