02. al-Albaaniy hakuwa Takfiyriy


Kusema kwamba al-Albaaniy alikuwa Takfiyriy mwenye kufuata madhehebu ya Sayyid Qutwub si sahihi al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Haifai kumkufurisha mtu anayetumbukia katika kitendo kinachopelekea katika kufuru mpaka tujue kuwa anaonelea kuwa ni halali.”[1]

al-Albaaniy akataja upokezi wa Ibn ´Abbaas (Rahimahu Allaah) pale alipokuwa anafasiri maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.” (05:44)

pale aliposema:

“Yule mwenye kukanusha aliyoteremsha Allaah amekufuru, yule mwenye kukubali na akaacha kuhukumu kwayo basi amedhulumu na ametenda dhambi nzito.”[2]

Ameyataja hayo Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) kupitia njia ya ´Aliy bin Abiy Twaalib na akamnasibishia nayo Ibn Jariyr. Kisha akasema:

“Kisha Ibn Jariyr akachagua kuwa Aayah inawakusudia watu wa Kitabu na yule anayepinga hukumu ya Allaah iliyoteremshwa katika Qur-aan.”[3]

Nimemsikia mwenyewe[4] al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) akisema:

“Haifai kwetu kumkufurisha mtu anayefanya kitendo kinachopelekea katika kufuru, kama vile kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah, mpaka tujue kuwa anafanya hivo kwa kuhalalisha. Akihalalisha hayo ndani ya moyo wake, amekufuru. Ama kuhalalisha kimatendo tu ni dhambi, sio kufuru inayomtoa mtu katika Uislamu.”

Wakati at-Twahaawiy aliposema:

“Hatumkufurishi yeyote kwa dhambi aliyotenda midhali hajaihalalisha.”

al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) akayawekea hayo taaliki na kusema:

“Bi maana kuyahalalisha kimoyo au kiimani. Vinginevyo kila dhambi ni yenye kuhalalishwa kimatendo. Kwa ajili hiyo ndio maana inatakiwa kutofautisha kati ya uhalalishaji wa kimatendo na wa kiitikadi. Yule mwenye kuhalalisha dhambi kimatendo ni dhambi inayostahiki kuadhibiwa ikiwa Allaah hakumsamehe mtu huyo. Mwishowe Allaah atamtoa Motoni. Tofauti na wanavyoonelea Khawaarij na Mu´tazilah ambao wanaonelea kuwa atadumishwa Motoni milele, hata kama kidhahiri wametofautiana kama inafaa kumwita kafiri au mnafiki. Hivi sasa kumezuka kundi jipya ambalo linawafuata hawa na wanawakufurisha wengi katika waislamu, ni mamoja wakawa wananchi au watawala. Limezuka Syria, Makkah… “

Amesema tena:

“Wana shubuha za Khawaarij juu ya yale maandiko yasemayo “Mwenye kufanya kitu kadhaa amekufuru”… Hapa kuna jambo linalotakiwa kufahamika; kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah inaweza kuwa kufuru inayomtoa mtu katika Uislamu kama ambavyo inaweza kuwa maasi, kubwa au ndogo… “[5]

Ameandika haya miaka thelathini iliyopita na bado yuko katika hali hiyo. Tazama kijitabu “at-Tahdhiyr min-al-Wuquu´ fiyt-Takfiyr”[6] ya al-´Urayniy ili ubainikiwe na uongo wa mtu huyu – Allaah amwongoze.

[1] Tazam ”Fitnat-ut-Takfiyr” ya al-Albaaniy, uk. 16

[2] Jaami´-ul-Bayaan (10/357).

[3] Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/119).

[4] Kutoka kwenye mkanda.

[5] Tazama maandishi ya chini ya ”Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah”, uk. 60

[6] Uk. 24

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fath ar-Rabbaaniy fiyd-Difaa´ ´an-ish-Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 22/01/2018